1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Rais Xi amwalika Putin kuzuru China mwaka huu

Sylvia Mwehozi
21 Machi 2023

Rais wa China Xi Jinping amesema hii leo kwamba amemwalika Rais wa Urusi Vladimir Putin kuzuru China mwaka huu, kabla ya duru ya pili ya mazungumzo kati ya viongozi hao wawili inayotarajiwa kufanyika leo mjini Moscow.

https://p.dw.com/p/4OyYq
Xi Jinping zu Besuch in Moskau
Picha: Russian Presidential Press Office/AP/picture alliance

Rais Xi aliwasili mjini Moscow siku ya Jumatatu na kisha kukutana na mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin katika Ikulu ya Kremlin kabla ya mazungumzo zaidi yaliyopangwa kufanyika Jumanne. Ziara ya Xi imetuma ujumbe mzito kwa viongozi wa nchi za magharibi kwamba juhudi zao za kuitenga Moscow kufuatia mapigano ya Ukraine, huenda zimegonga mwamba.

Mapema siku ya Jumanne, Rais Xi amekutana na waziri mkuu wa Urusi Mikhail Mishustin na kueleza kwamba "jana alimwalika rais Putin kuzuru China mwaka huu katika wakati ambao utakuwa mwafaka kwake".

Xi Jinping zu Besuch in Moskau
Rais wa China Xi Jinping na mwenyeji wake Rais Vladimir Putin mjini MoscowPicha: Russian Presidential Press Office/AP/picture alliance

Mataifa hayo mawili yaliyo na nguvu ya Urusi na China, yameitaja ziara ya siku tatu ya Xi kuwa fursa muhimu ya kuimarisha "urafiki wao usio na mipaka". China inaitizama Urusi kama chanzo cha mafuta na gesi kwa ajili ya uchumi wake unaohitaji nishati na kama mshirika katika kukabiliana na kile ambacho wote wanakiona kama uchokozi wa Marekani, udhibiti wa masuala ya kimataifa na adhabu isiyo ya haki kuhusiana na rekodi zao za haki za binadamu.

Ziara ya Xi inafanyika siku chache baada ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kutoa waranti ya kukamatwa kwa Putin huku Marekani ikilaani ziara hiyo na kusema kwamba inaonyesha kiasi gani Beijing inaipatia Moscow kinga ya kidiplomasia ya kutenda uhalifu zaidi.

Kulingana na ripoti za mashirika ya habari ya Urusi, Putin na Xi walisalimiana kama "marafiki wa dhati" mara walipokutana Kremlin na kufanya mazungumzo yasiyo rasmi kwa takribani masaa manne huku mazungumzo rasmi yakipangwa kufanyika siku ya Jumanne. Putin amemweleza Xi kuwa anayatizama mapendekezo ya China katika kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Ukraine kwa heshima. Xi kwa upande wake alimsifu Putin na kutabiri kwamba Warusi watamchagua tena hapo mwakani.

Russland | Zeremonie zur Annexion ukrainischer Gebiete | Mikhail Mishustin
Waziri mkuu wa Urusi Mikhail MishustinPicha: Grigory Sysoev/SNA/IMAGO

Wang Wenbin ni msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China kuhusu yaliyojitokeza anasema kuwa ; "Rais Xi Jinping alisisitiza kuhusu suala la Ukraine, kumekuwa na sauti za amani na zenye busara zaidi. Nchi nyingi zinaunga mkono kupunguzwa kwa mvutano, kutetea na kukuza mazungumzo ya amani, na kupinga kuongeza mafuta katika moto.China iko tayari kuendelea kuchukua jukumu la kuhimiza suluhisho la kisiasa juu ya suala la Ukraine."Rais Xi apongeza uhusiano wa China na Urusi

Naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vereshchuk aliliambia gazeti la Corriere della Sera la Italia kuwa Kyiv inasubiri uthibitisho ikiwa Xi atampigia simu Rais Volodymyr Zelenskiy kujadili pendekezo la Beijing la kuutatua mzozo unaoendelea.

China ilitoa pendekezo la kutatua mzozo wa Ukraine, pendekezo linalopuuzwa kwa kiasi kikubwa na nchi za Magharibi na kulitizama kama njama ya kumpatia muda zaidi Putin wa kukusanya tena majeshi yake na kuimarisha udhibiti wake kwenye ardhi iliyokaliwa.