1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto amteua Kindiki kuwa naibu mpya wa rais wa Kenya

18 Oktoba 2024

Bunge la Taifa la Kenya limepitisha jina la mrithi wa naibu wa rais zikiwa zimepita saa chache tangu kumuondowa Rigathi Gachagua kwa kura ya kutokuwa na imani naye.

https://p.dw.com/p/4lwg9
Makamu wa Rais mteule wa Kenya Profesa Kithure Kindiki
Makamu wa Rais mteule wa Kenya Profesa Kithure KindikiPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Bunge la Taifa la Kenya limepokea jina la mrithi wa naibu wa rais zikiwa zimepita saa chache tangu kumuondowa Rigathi Gachagua kwa kura ya kutokuwa na imani naye. Sasa wanapiga kura kumuidhinisha Kithure Kindiki, waziri wa usalama wa taifa, kuchukua nafasi ya naibu wa rais. Wakati huo huo, mawakili wa Rigathi Gachagua wamefika mahakamani kupinga uamuzi wa baraza la Seneti wa usiku wa kuamkia leo wa kumtimua.

Saa chache baada ya afisi ya naibu wa rais kuwa tupu, bunge la Taifa limepokea jina jipya la atakayeijaza nafasi hiyo nalo ni Kithure Kindiki. Spika wa bunge la Taifa Moses Wetangula alitangaza ujumbe huo wakati kikao maalum kilipoanza asubuhi ya Ijumaa (18.10.2024).

Kithure Kindiki ateuliwa kuwa naibu wa rais

Bunge laidhinisha jina la naibu wa rais Kithure Kindiki
Bunge laidhinisha jina la naibu wa rais Kithure KindikiPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Waziri wa usalama wa Taifa Kithure Kindiki ndiye atakayemrithi Rigathi Gachagua na bunge sasa linapiga kura kumpa ridhaa. Kikao cha kamati ya utaratibu wa bunge cha faragha kimefanyika asubuhi baada ya bunge kukutana kwa fursa maalum.

Kwa mujibu wa katiba, baada ya jina la mrithi wa naibu kuwasilishwa na rais, bunge la Taifa lina wajibu wa kumridhia au kumkatalia.

Hata hivyo uteuzi huo hauhitaji thuluthi mbili ya kura zote ili kupita. Baada ya hapo ataapishwa rasmi na kuanza kutimiza majukumu yake mapya.

Kithure Kindiki anaungwa mkono na viongozi 69 wa eneo la Mlima Kenya ambao walimpa ridhaa awawakilishe. Geoffrey Ruku ni mbunge wa Mbeere na mmoja wa viongozi waliomuunga mkono Kithure Kindiki kuwa mwakilishi wao na amempongeza kwani, "Kithure Kindiki ni mchapa kazi na ana uwezo wa kuliunganisha taifa.Huu ni wakati mwafaka kwa wakenya kuungana na kuja pamoja kwa manufaa ya taifa," anafafanua.

Mtazamo huo umehanikiza hadi maeneo mengine mbali na Mlima Kenya. Tindi Mwale ni mbunge wa Butere na amefurahishwa na hatua hiyo, "Huu ni uteuzi muhimu kwetu sote,Kithure Kindiki ni msomi, amehudumu kama waziri wa usalama wa taifa kwahiyo anawaelewa wakenya."

Gachagua mahakamani kujikomboa

Seneti yamtimua naibu rais wa Kenya Rigathi Gachagua
Seneti yamtimua naibu rais wa Kenya Rigathi GachaguaPicha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Yote hayo yakiendelea, katika hatua za mwisho za kujikomboa, mawakili wa Rigathi Gachagua wamekimbilia mahakamani kutia guu hatua ya kumtangaza mrithi wake katika afisi ya naibu wa rais. 

Kwa kufuata taratibu za dharura, wakili mkongwe Paul Muite anashikilia kuwa mashtaka yaliyomsulubisha Rigathi Gachagua mbele ya bunge la Taifa na baraza la Senate hayana mashiko.

Kwa mujibu wa wakili Paul Muite, baraza la Senate lilitakiwa kutoegemea upande wowote lilipokuwa linatathmini mashtaka hayo ya ufisadi na kukiuka katiba na hivyo ushahidi uliotolewa ulikuwa na walakini. Kauli hizo zinaungwa mkono na kiongozi wa chama cha upinzani cha Wiper Demokratik Kalonzo Musyoka aliyemtembelea Rigathi Gachagua hospitalini mtaani Karen na ,"Tumemuona.Anaendelea vizuri na tunamuombea afueni ya haraka. Hata hivyo nawapongeza maseneta waliosisitiza msimamo wao wa kumbandua Gachagua.Lakini kisheria kuna matatizo yaliyotokea na muhimu kuyaangazia kwa kina."

Kukamilika kwa ndoto ?

Wakati bunge linaendelea na taratibu za kumuidhinisha Kithure Kindiki kuwa naibu wa rais mpya, mawakili wa Rigathi Gachagua wanasaka mbinu ya kuuzuwia mchakato wa kumuhoji na kumpa ridhaa.

Kithure Kindiki amehudumu kama Waziri wa usalama wa taifa na seneta wa kaunti ya Tharaka Nithi kwa mihula miwili.Itakumbukwa kuwa kabla ya kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022, Kithure Kindiki alikuwa mmoja ya waliotazamiwa kuwa mgombea wake mwenza.

Mwenyewe Rigathi Gachagua amelazwa kwenye hospitali ya Karen baada ya kupata maumivu makali ya kifua jambo lililomzuwia kujitetea mbele ya baraza la senate alikoshtakiwa.