Rwanda yachukua wakimbizi 500 waliokwama Libya
11 Septemba 2019Mjumbe maalumu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR katika eneo la Mediterrania ya Kati Vincent Cochetel amesema wakimbizi 500 watapelekwa nchini Rwanda, kufuatia makubaliano yaliyosainiwa kati ya Rwanda na Umoja wa Afrika.
Conchetel aliuambia wakfu wa Reuters kabla ya kutangazwa kwa mpango huo kwamba, "Rwanda imesema idadi hiyo inaweza kuongezeka kutoka 500, iwapo wataridhika na uendeshwaji wa mpango huo".
Libya kwa muda mrefu imekuwa njia kuu ya waafrika wanaokimbia vita na umasikini kwenye nchi zao na kutorokea Ulaya kutafuta maisha bora, tangu kiongozi wa taifa hilo Muammar Gaddafi alipoondolewa madarakani kufuatia mapinduzi yaliyoungwa mkono na jumuiya ya Kujihami ya Ulaya, NATO mnamo mwaka 2011.
Mjini Geneva, msemaji wa UNHCR, Babar Baloch hapo jana alizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na makubaliano hayo akisema "Kundi la kwanza litatakiwa kuwa na wakimbizi 500, lakini hiyo sio idadi kamili, ni kundi la kwanza la watu 500 watakaoondolewa Libya na kupelekwa Rwanda. Chini ya makubaliano haya, serikali ya Rwanda itapewa, lakini pia itatoa ulinzi kwa wakimbizi na waomba hifadhi ambao hivi sasa wanashikiliwa kwenye vituo huko Libya."
Rwanda tayari inahifadhi wakimbizi 150,000 wa DRC na Burundi.
UNHCR imesema kuna takriban wakimbizi 4,700 kutoka mataifa mbalimbali ambayo ni pamoja na Eritrea, Somalia, Ethiopia na Sudan wanaoshikiliwa kwenye vituo hivyo.
Chini ya makubaliano hayo, wakimbizi wanaotaka kuondoka watasafirishwa kwa ndege hadi Rwanda na watahifadhiwa kwenye vituo vya muda vilivyopo kwenye viunga vya Kigali.
Kipaumbele kitatolewa kwa wale walio katika mazingira ya hatari zaidi na miongoni mwao ni watoto wasio na wazazi ama walezi, walemavu na wazee. Wengi wa wakimbizi watakuwa ni wale wanaotoka kwenye mataifa ya Upembe wa Afrika.
Kulingana na Cochetel, Rwanda imeahidi kutoa nafasi kwa ajili ya wakimbizi hao, na kuwapatia hadhi pamoja na hati za ukaazi. Aidha imesema itawatambua kisheria kuwa ni wakimbizi.
Kulingana na Cochetel, mfadhili mkuu wa mpango huo ni Umoja wa Ulaya, lakini pia Umoja wa Afrika ulipewa dola miioni 20 na Qatar ili kuunga mkono mchakato wa kuwajumuisha tena wakimbizi na wahamiaji wa Afrika.
Rwanda ambayo inakaliwa na idadi kubwa ya watu, tayari inahudumia takriban wakimbizi 150,000 kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi.