1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rwanda yaruhusu bangi itumike kimatibabu na kiuchumi

Sylvanus Karemera14 Oktoba 2020

Wananchi nchini Rwanda wamepokea kwa hisia tofauti mpango wa serikali yao wa kuruhusu kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya  kimatibabu na kiuchumi. Kwa mujibu wa sheria matumizi ya bangi Rwanda ni marufuku

https://p.dw.com/p/3jw1F
USA Cannabis-Anbau im Gewächshaus
Picha: Richard Vogel/AP/picture alliance

Hisia hizi mseto miongoni mwa wananchi zinatolewa siku moja baada ya baraza la mawaziri kupitisha kwa kauli moja mpango wa kuanzisha kilimo cha bangi nchini Rwanda, lakini kwa sababu za kimatibabu na kwa mauzo ya nje. Hii ikawa sababu ya baadhi ya wananchi kama Kwizera Aimant kuibua maswali

"Ni uamuzi mzuri kwa uchumi wa Rwanda kwa sababu hii inayoendelea lakini tatizo ni kwamba jambo hili litaathiri watu wengi kwa sababu sheria ni wazi zinapiga marufuku ya watu kutumia bangi, na huku serikali ndiyo sasa imeamua kulima bangi hiyo..Mimi nadhani wasingekimbilia kuchukua maamuzi ya haraka, kwanza wangechukua muda na kuwafafanulia wananchi kuliko kuchukua maamuzi ya haraka"

USA New York | CBD Snack
Pipi zenye bangiPicha: picture-alliance/Photoshot

Serikali imeshikilia kwamba kilimo hiki kitaendeshwa kwa mujibu wa sheria na lengo lake linahusu maslahi ya kiuchumi na afya hasa kuviwezesha viwanda vya kutengeneza dawa na kemikali nyingine kuhusu huduma ya mwanadamu kupata malighafi ili kutoa matibabu hasa watu wenye magonjwa sugu.

Waziri wa afya wa Rwanda Dr Daniel Ngamije amesema kilimo cha bangi kitakuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa Rwanda lakini kubwa zaidi kuhusu huduma bora katika sekta ya afya. Soma Zambia yahalalisha usafirishaji wa bangi kukuza uchumi

"Ukianzia na kilimo cha chai na kahawa kilimo hiki tunachokizungumzia kitatupatia nafasi ya kutuma bidhaa hii nje ya nchi kama zilivyo bidhaa nyingine za mazao mbalimbali, lakini haya yataleta faida hasa kwenye sekta ya afya. Ni kilimo ambacho kitaendeshwa kwa usalama mkubwa kabisa kwa sababu mkulima yeyote anayehitaji kuwekeza atahitaji kuwa na kibali maalum, na mahali pa wazi pa kuendeshea kilimo hicho ambacho mazao yake yatauzwa nchi za nje kwa ajili ya viwanda vya madawa."

Mkakati wa serikali ni kuhakikisha pato litokanalo na bidhaa zinazouzwa nchi za nje linapanda kutoka dola laki 465 kwa sasa hadi dola za Marekani bilioni moja za Marekani ifikapo mwaka 2024.

Kanada | Cannabisforscher Igor Kovalchuck
Daktari Igor Kovalchuck,mtafiti wa bangiPicha: privat

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya taifa ya maendeleo RDB ambayo kazi yake ni kuratibu na kuhamasisha uwekezaji wa kigeni nchini Bi Clare Akamanzi amesema kuanzisha kwa kilimo cha bangi ni fursa nyingine ya maendeleo ya kiuchumi ambayo serikali imeyajenga sasa na kwamba huenda ikawa mojawapo ya mikakati ya kuinua kiwango cha ajira.Bangi ruksa kwa wagonjwa Ujerumani

"Mavuno ya zao hili kwa kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta moja yanafikia karibu dola milioni 10 za Marekani.Ukilinganisha kwa mfano kilimo cha maua, mavuno kwa ekari moja utapata milioni tatu dola za Marekani, nadhani unaona tofauti iliyopo kati ya milioni tatu na miliyoni kumi.Ni faida kubwa kwa uchumi wa taifa na ajira kwa ujumla, na hapa tunazungumzia mamia ya watu wengi wanaokosa ajira.Mimi najikita kwa faida hizi juu ya afya,uchumi pamoja na kutoa ajira."

Mpaka sasa serikali haijabainisha ni eneo gani la nchi ambako kutaendeshwa kilimo hiki cha bangi wala kutangaza  hasa ni wakati gani kitakapoanzishwa. Kwa mujibu wa sheria ya sasa, kulima na kutumia bangi ni kosa la jinai.