Save the Children yasema wafanyakazi wake wameuawa Myanmar
28 Desemba 2021Wapiganaji wanaopambana dhidi ya utawala huo wa kijeshi walisema waligundua miili zaidi ya 30 iliyounguzwa, ikiwemo ya wanawake na watoto, kwenye barabara kuu jimboni Kayah, ambako waasi wanaopigania demokrasia wamekuwa wakipambana dhidi yajeshi.
Save the Children imesema wawili kati ya wafanyakazi wake walizingirwa katika tukio hilo na walikuwa hawajulikani waliko.
Myanmar imekuwa katika machafuko tangu mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Februari, ambapo watu zaidi ya 1,300 wameuawa katika ukandamizaji wa vikosi vya usalama, kulingana na shirika la ufuatiliaji.
Soma pia: Wapinzani waanzisha mgomo baridi Myanmar
Makundi yanayojinadi kuwa "vikosi vya ulinzi wa watu" yamechipuka kote nchini humo kupambana dhidi ya utawala wa kijeshi, na kulitumbukiza jeshi katika mkwamo wa umuagaji damu na mauaji ya visasi.
Hii leo Save the Children imethibitisha katika taarifa kuwa wafanyakazi wake wawili wa kiume walikuwa miongoni mwa watu wasiopungua 35, wakiwemo wananawake na watoto, waliouawa.
Taarifa hiyo imesema jeshi liliwalaazimisha watu kutoka kwenye magari yao, kuwakamata baadhi, kuwaua wengi na kisha kuchoma miili yao.
Utawala wa kijeshi wa Myanmar ulisema awali kwamba wanajeshi walishambuliwa katika mji mdogo wa Hpruso siku ya Ijumaa, baada ya kujaribu kusimamisha magari saba yaliokuwa yanaendeshwa kwa namna inayotiliwa mashaka.
Soma pia:Myanmar: Suu Kyi afungwa miaka 4 Jela
Msemaji wa wa utawala huo Zaw Min Tun, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba wanajeshi waliuwa idadi isiyotajwa ya watu katika makabiliano yaliofuatia.
Shirika la ufautiliaji la Myanmar Witness limesema lilithibitisha ripoti za vyombo vya habari vya ndani pamoja na maelezo ya mashuhuda kwamba watu 35, wakiwemo watoto na wanawake walichoma na kuuawa na jeshi katika shambulio hilo.
Miito ya uchunguzi huru
Data za satelaiti zilionyesha kuwa moto ulitokea majira ya saa saba mchana siku ya Ijumaa mjini Hpruso.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaeshughulikia masuala ya kiutu Martin Grifiths baadae alisema alishutushwa na ripoti za mauaji hayo, na kuitaka serikali iendesha uchunguzi.
Ubalozi wa Marekani pia ulielezea kushtushwa na mauaji hayo kupitia ukurasa wa Twitter.
Save thr Children, ambayo ina wafanyakazi karibu 900 nchini Myanmar, baadae alisema imesitisha operesheni zake katika jimbo la Kayah na maeneo mingine kadhaa.
Mnamo mwezi Oktoba shirika hilo lilisema ofisi zake katika mji wa magharibi wa Thantlang ziliharibiwa katika mashambulizi ya utawala wa kijeshi ambayo yaliharibu nyumba kadhaa kufuatia makabiliano na kundi linalopinga utawala huo.
Chanzo: Mashirika ya Habari