1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz ayaweka mezani ´masuala mazito´ ziara yake China

15 Aprili 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz yuko China kwa ziara inayoangazia mahusiano ya kiuchumi yanayozidi kuzorota baina ya mataifa hayo pamoja na tofauti zao kufuatia uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4ejsa
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amewasili nchini China siku ya Jumapili:14.04.2024Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Ziara ya Scholz ilianzia kwenye kitovu cha viwanda, mjini Chongqing ambako pamoja na ujumbe wake wa mawaziri na viongozi wa kibiashara walitembelea kampuni inayofadhiliwa kwa kiasi fulani na ujerumani na maeneo mengine ya eneo hilo ambalo ni kitovu cha kuzalisha magari nchini China.

Soma pia: Kansela Olaf Scholz kuanza ziara ya siku tatu nchini China

Katika ziara hiyo ya siku tatu, Scholz pia aliutembelea mji wa Shanghai ambao ni kitovu cha biashara kabla ya kwenda mji mkuu Beijing, atakapokutana na Rais Xi Jinping na Waziri Mkuu Li Qiang.

Magari yanayotengenezwa Ujerumani kama BMW na Volkswagen yanategemea kwa kiasi kikubwa soko la China, licha ya Beijing kuiunga mkono Urusi, hatua inayoibua msuguano kati yake na mataifa ya magharibi.

Ujerumani inafaidika na bidhaa kutokana na mahitaji ya bidhaa kutoka  China kuanzia magari hadi kemikali lakini mahusiano ya nchi hizo mbili yanayumba kufuatia kampuni za Ujerumani kusema zinakumbana na vizingiti visivyo vya haki katika biashara zao nchini China.  

Kansela huyo wa Ujerumani anamalizia ziara yake ya siku tatu nchini China hii leo, aliyoandamana na ujumbe mkubwa wa wafanya biashara na wakurugenzi kadhaa wa kampuni za kijerumani. Katika ziara yake hiyo Scholz pia aliizungumzia Taiwan bila ya kuitaja moja kwa moja akiitahadharisha China kwamba kuionea nchi ndogo ni makosa.