1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

Scholz na Xi kujadili juu ya China kuisaidia Urusi kijeshi

Hawa Bihoga
15 Aprili 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema atamuonya Rais Xi Jinping, dhidi ya kile alichokitaja kutoa msaada wa kijeshi kwa Urusi. Scholz na Xi wanatarajiwa kukutana siku ya Jumanne mjini Beijing.

https://p.dw.com/p/4eoJt
China Shanghai | Kansela Olaf Scholz akizungumza na wanafunzi wa chuo kikuu cha Tongji.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz katika mazungumzo yake na wanafunzi wa chuo kikuu cha Tongji.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Katika mazungumzo yake hapo kesho yanatazamiwa kuvuta nadhari ya kimataifa huku  mzozo wa Ukraine ukiwa umeendelea kuwa changamoto kwa mataifa ya Ulaya, Kansela Scholz atatumia ziara hiyo kuzungumza na rais Xi Jinping kuhusu uungaji mkono wa China katika uchumi wa Urusi katika kipindi cha miaka miwili baada ya Moscow kufanya uvamizi kamili nchini Ukraine.

Kabla ya kuwasili nchini China Kansela Scholz aliandika katika mtandao wa X zamani Twitter kwamba amefanya mazungumzo na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, kuhusu mashambulizi "makubwa" ya anga ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nishati nchini Ukraine na kuendelea na msisitizo wake wa mara zote kwamba Berlin "itaendelea kuiunga mkono Kyiv bila kutetereka."

Soma pia:Scholz ayaweka mezani ´masuala mazito´ ziara yake China

Akiwa mjini Shanghai ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika chuo kikuu cha Tongji, kiongozi huyo amesema, Urusi inaendesha vita vya ushindani dhidi ya Ukraine, lakini haipaswi kupata msaada ili kufanikiwa katika vita hivyo vilivyodumu kwa takriban miaka miwili sasa.

"Shambulio la Urusi dhidi ya Ukraine sio suala linaloihusu Ulaya peke yake, sababu kadri itakavyoendelea kushambulia, itazidi kuwa tishio kwa amani na usalama wa kila pahala katika sayari hii." alisema Scholz.

Aliongeza kuwa "kwa sababu hiyo nitazungumza juu ya vita hivi ambavyo Urusi inaendesha dhidi ya Ukraine na ninasisitiza kwamba hakuna anayepaswa kuisaidia Urusi ili kufanikiwa."

Kuimarika biashara kati ya Beijing na Moscow

Tangu Urusi ilipofanya uvamizi kamili nchini Ukraine mnamo Februari 2022, China ambae ni mshirika wa karibu wa Moscow ilikataa kukosoa uchukozi huo hadharani.

Beijing imeendelea kuimarisha mahusiano yake ya kibiashara na Moscow na mataifa hayo mawili yanafanya luteka za pamoja za kijeshi.

Juma lililopita Marekani iligundua kuwa China imeongeza mauzo yake ya zana mbalimbali kwa Urusi ili kuisaidia katika oparesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine.

Ujerumani: Hatutaiacha Ukraine kwenye vita peke yake

Aidha Scholz alionesha wasiwasi wake juu ya uvamizi wa China dhidi ya Taiwan, kisiwa kinachojitawala ambacho Beijing inasema ni sehemu ya himaya yake.

Soma pia:Scholz ataka ushindani sawa biashara ya magari na China

Kando na masuala ya siasa na diplomasia Kansela Scholz ametolea mwito wa kuwepo na ushindani wa haki katika masuala ya kibiashara na China huku akionya juu ya utupaji wa taka na uzalishaji uliopitiliza wa bidhaa.

Ziara ya Scholz inafanyika wakati China imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa Ujerumani kwa mwaka wa nane mfululizo huku bidhaa na huduma kwa pande zote mbili zimezalisha kiasi cha yuro bilioni 254.1, kiwango ambacho ni zaidi Ujerumani ilichofanya na Marekani.

Hii ni ziara ya pili ya Scholz nchini China tangu awe Kansela mnamo mwaka 2021. Ziara yake ya siku moja aliifanya mwaka 2022 chini ya vizuizi vikali vya UVIKO-19.