Serikali ya Afghanistan kushiriki mazungumzo yote ya amani
13 Machi 2021Taarifa hizo zimetolewa Jumamosi na Baraza la Usalama la Taifa la Afghanistan. Mkutano wa kilele unaoungwa mkono na urusi umepangwa kufanyika Alhamisi ijayo ya Machi 18 mjini Moscow, huku ule wa Marekani ukiwa umepangwa kufanyika nchini Uturuki mwezi ujao wa Aprili.
Akizungumza kwenye mkutano wa kila wiki na waandishi habari, Mshauri wa Usalama wa Taifa nchini Afghanistan, Hamdullah Mohib amesema nchi yake imeanza kuwaandaa pamoja wajumbe watakaohudhuria mikutano yote miwili.
Hata hivyo, Mohib amesema ukubwa wa ujumbe wa serikali ya Afghanistan utategemea na idadi ya wawaklishi watakaopelekwa na kundi la wanamgambo wa Taliban pamoja na wawakilishi kutoka mataifa mengine.
Aidha, msemaji wa Taliban ameliambia shirika la habari la Ujerumani, DPA kwamba kundi hilo bado halijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu kuhudhuria kwenye mikutano hiyo.
Barua za mwaliko ya mikutano hiyo ya kilele zimetumwa kwa serikali ya Afghanistan, viongozi wa kisiasa, kundi la Taliban na wawakilishi wa Marekani, China na Pakistan.
Juhudi za kidiplomasia za Urusi zinafanyika wakati Marekani nayo ikiendeleza juhudi za kuharakisha mchakato wa amani ya Afghanistan kabla wanajeshi wake hawajaondoka nchini humo Mei Mosi.
Soma zaidi: Taliban, serikali warejea kwenye mazungumzo ya amani
Mwaka uliopita, Marekani ilisaini makubaliano ya kuwaondoa wanajeshi wake na Taliban kufuatia uvamizi wa kijeshi wa nchi hiyo miaka 19 iliyopita, huku kundi hilo nalo likitangaza rasmi kusitisha ghasia na kushiriki katika mazungumzo ya amani ya Afghanistan.
Marekani yataka mkutano wa ngazi ya juu
Serikali mpya ya Marekani ya Rais Joe Biden ilipendekeza rasmi kufanyika kwa mkutano wa ngazi ya juu utakaoongozwa na Umoja wa Mataifa kati ya Taliban na wanasiasa wa Afghanistan nchini Uturuki mwezi ujao wa Aprili ili kukamilisha makubaliano ya amani kwa kuzungumzia suluhu ya kisiasa na kusitisha mapigano.
Mazungumzo ya amani kati ya Taliban na wawakilishi wa serikali ya Afghanistan huko Qatar yamekwama katika miezi ya hivi karibuni, huku kukiwa hakuna maendeleo yoyote yanayoonekana.
Wakati huo huo, takriban watu wanane wameuawa baada ya mlipuko mkubwa wa bomu la kutegwa kwenye gari kutokea magharibi mwa Afghanistan. Shambulizi hilo lililotokea mapema Jumamosi likiyalenga makao makuu ya jeshi la polisi kwenye mji wa Herat limesababisha uharibifu wa nyumba na maduka kadhaa.
Msemaji wa gavana wa jimbo la Herat, Jailan Farhad amesema watu wengine 47 wamejeruhiwa katika shambulizi hilo, huku watoto na maafisa wa usalama wakiwa ni miongoni mwa waliouwawa.
Msemaji wa kundi la wanamgambo wa Taliban ambalo wapiganaji wake hufanya mashambulizi kwenye eneo la magharibi mwa Afghanistan amekanusha kundi hilo kuhusika na shambulizi la Jumamosi.
Hata hivyo, Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani, amelishutumu kundi la Taliban kwa kile alichokitaja kuwa muendelezo wa vita haramu na machafuko dhidi ya raia.
Saa chache baada ya kutokea shambulizi hilo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vikali ongezeko la ''kutisha'' la mashambulizi nchini Afghanistan ambayo yanawalenga raia.
(DPA, AP, Reuters)