Taliban, serikali warejea mazungumzo ya amani ya mashaka
25 Februari 2021Msemaji wa kundi la Taliban Dk. Mohammad Naeem aliandika katika ukurusa wake wa Twitter siku ya Jumatatu usiku kwamba mazungumzo yalikuwa tayari yamekwishaanza katika jimbo la mashariki ya kati nchiniQatar, ambako kundi hilo lina afisi ya kisiasa.
Hakutoa taarifa zozote mbali na kusema mazungumzo yalifanyika katika mazingira mazuri ya kirafiki, kutolewa ahadi kwamba yanatakiwa kuendelea na tangazo kuwa suala la kwanza la kipaumbele litakuwa kuweka agenda.
Wakati mazungumzo yaliposambaratika ghafla mnamo mwezi Januari, siku chache baada ya kuanza, pande zote mbili ziliwasilisha orodha ya matakwa yao kwa ajili ya agenda.
Kazi iliyopo sasa ni wajumbe wa pande zote mbili kufanya uchanganuzi wa orodha hizo, wakumbaliane masuala ya kuyajadili na kuainisha wataanza na lipi na kuendelea na yapi.
Marekani yapitia upya mkataba na Taliban
Kipaumbele kwa serikali ya Afghanistan, Marekani na Jumuiya ya kujihami yaNATO ni kupunguzwa kwa kiwango kikubwa machafuko kutakakosaidia kusitisha kabisa mapigano. Taliban wamesema suala hilo linajadilika, lakini mpaka sasa wamepinga usitishaji wowote haraka wa mapigano.
Marekani inadurusu upya mkataba wa amani wa Februari 2020 uliosainiwa kati ya utawala uliopita wa rais wa zamani Donald Trump na Taliban, unaotaka wanajeshi wa kimataifa waondoke Afghanistan ifikapo Mei mosi.
Soma pia: Nchi wafadhili kutoa dola bilioni 12 kuisaidia Afghanistan
Taliban wamepinga mapendekezo ya kuurefusha japo kifupi muda huo, lakini makubaliano yanakaribia kufikiwa nchini Marekani kuichelewesha tarehe hiyo ya kuondoka vikosi vya kimataifa.
Hata kuna pendekezo la kikosi kidogo cha ujasusi kubaki kitakachokuwa na kibarua kipevu cha kupambana na ugaidi na kikundi chenye mafungamano na kundi la dola la kiislamu IS chenye makao yake makuu mashariki mwa Afghanistan.
Lakini hadi sasa Marekani na NATO hawajatangaza uamuzi kuhusu hatma ya wanajeshi takriban 10,000, wakiwamo wanajeshi 2,500 wa Marekani ambao bado wako nchini Afghanistan.
Biden asisitiza suluhisho la kisiasa
Utawala wa rais Joe Biden umesisitiza suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa muda mrefu wa Afghanistan, kumbakisha Zalmay Khalilzad, mtu aliyesimamia mkataba wa amani kati ya Marekani na Taliban na mpaka sasa wamejiepusha kutoa kauli kuhusu njia ya kufuata na mipango ya baadaye.
Kuanza tena kwa mazungumzo mjini Doha kunafuatia harakati za kidiplomasia zikiwamo ziara za maafisa kwenda Pakistan na Mkuu wa jeshi Jenerali Qamar Javed Bajwa.
Pakistan inaonekana kuwa na umuhimu mkubwa katika kuwashawishi Taliban kurejea kwenye meza ya mazungumzo, lakini pia katika kulishikiza vuguvugu hilo ambalo uongozi wake una makao yake makuu nchini Pakistan, kupunguza machafuko Afghanistan.
Huku maelezo ya kina kuhusu mkutano yakikosekana, suala la Afghanistan lilitawala mazungumzo na maafisa walio karibu na mazungumzo hayo wamesema kupunguzwa kwa machafuko na hatimaye usitishwaji mapigano yalijadiliwa sana.
Soma pia: Ripoti: Mashambulizi ya Taliban yanaongezeka
Pakistan, ambayo pia ni nyumbani kwa wakimbizi milioni 1.5 wa Afghanistan imesema mara kwa mara kwamba suluhisho pekee nchini Afghanistan ni la kisiasa na siku za nyuma imepongezwa kwa kuwashawishi Taliban kukaa katika meza ya mazungumzo.
Masuala yaliyo mbele ya Taliban na serikali ya Afghanistan ni pasuakichwa na haijabainika wazi dhahiri shahiri ikiwa nchi yoyote ina ushawishi wa kutosha na kila upande kuweza kulazimisha mkataba wa amani utakaodumu muda mrefu.
Chanzo: AP