1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban kuendelea kuzungumza na serikali ya Afghanistan

Josephat Charo
3 Desemba 2020

Serikali ya Afghanistan na wajumbe wa Taliban wamefikia makubaliano ya awali leo kuendelea mbele na mazungumzo ya kutafuta amani. Ni makubaliano ya kwanza kuwahi kuandikwa katika kipindi cha miaka 19 ya vita.

https://p.dw.com/p/3mB5B
Katar Doha | Mike Pompeu, US-Außenminister & Abdul Ghani Baradar, Taliban
Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Makubaliano hayo yanaainisha njia itakayofuatwa kendelea na mazungumzo na yanachukuliwa kuwa ufanisi muhimu kwa sababu yatawaruhusu wapatanishi kuendelea kujadili masuala nyeti yakiwemo mazungumzo kuhusu usitishwaji mapigano, wakati ambapo mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban dhidi ya vikosi vya serikali ya Afghanistan yameendelea kuchacha.

Nader Nadery, mwanachama wa timu ya upatanishi ya serikali ya Afghanistan, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba utaratibu mzima na utangulizi wa mashauriano umeshakamilika na kuanzia sasa, mazugumzo yataanza kuhusu ajenda.

Msemaji wa kundi la Taliban amethibitisha kufikiwa makubaliano hayo katika ukurasa wa twita. Taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya kikao cha mjini Doha imesema "kamati ya pamoja imepewa jukumu la kuandaa rasimu ya mada kwa ajili ya ajenda ya mazungumzo ya amani"

Brüssel Jens Stoltenberg NATO-Generalsekretär
Picha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami ya NATO, Jens Stoltenberg, ameyapongeza makubaliano hayo ya Doha akiyataja kuwa hatua moja muhimu kuelekea suluhisho la amani la kisiasa la muda mrefu kwa mzozo na vita Afghanistan na washirika wote wa jumuiya hiyo wanauunga mkono kikamilifu mchakato wa amani. Stoltenberg amesema sasa wanataka kuona ufanisi zaidi.

"Sichukulii juu juu changamoto na vitisho vya vikwazo na hali ya kuvunja moyo kadri tunavyosonga mbele. Lakini nina hakika njia pekee ni mazungumzo yanayoendelea kati ya makundi ya Afghanistan na kwa hivyo tunayaunga mkono. Tunafahamu fika yatakuwa magumu, lakini ndilo chaguo pekee kwa wote wanaotaka amani Afghanistan."

Ni hatua muhimu ya kusonga mbele

Makubaliano hayo yanakuja baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo mjini Doha, Qatar, yaliyohimizwa na kusimamiwa na Marekani, licha ya machafuko yanayoendelea Afghanistan. Mjumbe wa Marekani aliyeyasimamia mazungumzo hayo, Zalmay Khalilzad, amesema Taliban na wajumbe wa serikali ya Afghanistan wamefanikiwa kumaliza mkwamo wa miezi mitatu na wamekubaliana juu ya sheria na kanuni za majadiliano.

Afghanistan Friedensgepräche in Doha
Picha: Hussein Sayed/AP/dp/picture alliance

Khalildad aidha amesema kuna waraka wa kurasa tatu uliosainiwa na kuwahimiza wajumbe wa Taliban na serikali waanze mazungumzo washauriane kuhusu mpango wa siasa na usitishwaji mapigano.

Waraka huo utatumika kama msingi wa mazungumzo yanayoendelea nchini Qatar ambako Taliban wameweka ofisi yao ya kisiasa. Usitishwaji mapigano, haki za wanawake na makundi ya wachache na mageuzi ya katiba yanatarajiwa kupewa kipaumbele katika ajenda, lakini pia suala la kuhakikishiwa ulinzi maelfu ya wapiganaji wa Taliban wanaoweka chini silaha na kuvunjwa kwa makundi ya waasi watiifu kwa wababe wa kivita wa mjini Kabul, ambao wengi wao wanaegemea upande wa serikali au wanasiasa wa upinzani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Mike Pompeo, ameyasifu makubaliano hayo akisema watashirikiana na pande zote husika kupunguza machafuko Afghanistan.

Vyanzo: reuters, ap