Serikali ya Sudan yalaani vikwazo dhidi ya al-Burhan
17 Januari 2025Vikwazo hivyo vilivyotangazwa siku ya Alhamisi dhidi ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan, vimelalamikiwa na serikali ya kijeshi inayosema kwamba havikuzingatia misingi ya haki na uwazi.
Wizara ya mambo ya nje ya Sudan imesema, uamuzi huo wa Marekani hauwezi kuhalalishwa kivyovyote vile kwa madai ya taifa hilo kubwa ya kutoegemea upande wowote, taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Sudan imesema hatua hiyo ni sawa na kuwaunga mkono wanaofanya mauaji ya kimbari.
Mnamo siku ya Alhamisi, wizara ya fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo dhidi ya kiongozi wa kijeshi wa Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, na kutoa lawama kwa jeshi kwa kushambulia shule, masoko na hospitali na pia kutumia kuwanyima watu chakula kama silaha ya vita.
Soma Pia: UN yaonya kuhusu mashambulizi ya kulipiza kisasi Sudan
Vikwazo dhidi ya Burhan vimetolewa katika muda wa wiki moja baada ya Marekani kumwekea vikwazo kiongozi wa vikosi vya RSF, Mohamed Hamdan Daglo, ambaye vikosi vyake vinalaumiwa kwa mauaji ya halaiki.
Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Sudan imesema baada ya miezi 21 ya vita kati ya jeshi na vikosi vya RSF kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan anapambana kwa ajili ya kuwalinda watu wa Sudan dhidi ya njama ya mauaji ya kimbari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayemaliza muda wake Antony Blinken amesema anasikitika kwa kushindwa kwa utawala unaoondoka kuvimaliza vita vya kikatili vya nchini Sudan.
Maelfu ya watu wameuawa tangu mwezi April mwaka 2023, vilipozuka vita kati ya jeshi kuu la Sudan na vikosi vya RSF. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makazi yao na wakati huo huo vita hivyo vimewatumbukiza maelfu ya watu katika baa la njaa.
Pande zote mbili zimelaumiwa kwa kuwalenga raia na pia kushambulia kwa makombora kwenye maeneo ya makazi, huku vikosi vya RSF vikibebeshwa lawama ya kulenga kimakusudi kuiangamiza jamii ya kabila fulani, unyanyasaji wa kijinsia uliopangwa na kuizingira miji.
Soma Pia: RSF imefanya mauaji ya kimbari - Marekani
Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, anayemaliza muda wake baada ya kuhudumu kwenye baraza la kijeshi la Sudan, aliapishwa mbele ya mkuu wa mahakama ya nchi hiyo mnamo Agosti 21, mwaka 2019 kama mkuu wa Baraza Kuu jipya lililoundwa hivi karibuni.
Chanzo: AFP