1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya umoja wa kitaifa Sudan Kusini hati hati

Sylvia Mwehozi
30 Oktoba 2019

Upinzani nchini Sudan Kusini umeishutumu serikali kwa kushindwa kufanikisha mkataba wa amani na kutoa wito wa kuchelewesha kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa kipindi cha miezi sita.

https://p.dw.com/p/3SD8M
Südsudan Unterzeichnung Friedensabkommen in Juba
Picha: Reuters/S. Bol

Kulingana na msemaji wa kiongozi wa zamani wa waasi Puok Both Buluang, Riek Macharhaamini kama ataweza kujiunga na serikali ya Umoja wa kitaifa ifikapo Novemba 12, ikiwa ni tarehe ya mwisho iliyokubaliwa mwezi Septemba baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo, makubaliano yaliyovunjika ya usitishaji mapigano na shinikizo kutoka Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi za kikanda.

Akizungumza baadae katika hafla ya kitaifa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, hakujibu moja kwa moja kauli iliyotolewa na Machar, lakini alisema kwamba pande zote katika makubaliano hayo zimejizatiti katika uundwaji wa serikali ya umoja ifikapo Novemba 12 na jumuiya ya kimataifa inatarajia hilo kutokea.

"Ninataka kuukaribisha upinzani na kusahau machungu yote", alisema Kiir. Hapakuwa na taarifa ya haraka kutoka kwa nchi ambazo zilisaidia kufanikisha makubaliano hayo. Maafisa wa Marekani walisema mwezi huu kwamba hawatakubali muda zaidi kucheleweshwa na huenda wakaiwekea Sudan Kusini vikwazo ikiwa tarehe ya mwisho itapita.

Südsudan -  Riek Machar und  Salva Kiir
Viongozi hasimu wa Sudan KusiniPicha: Reuters/M. N. Abdallah

Upinzani umeitaka serikali kutoa fedha iliyoahidi katika kutekeleza makubaliano, na kuongeza kwamba miezi sita itatoa mwanya wa kuyatatua masuala kadhaa yaliyosalia. Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya vita na kisha ikatumbukia katika mgogoro wake yenyewe mwishoni mwa 2013 baada ya Kiir kumfukuza Machar kama makamu wake wa rais.

Vikosi tiifu kwa viongozi wote wawili vilipambana mjini Juba mwezi Desemba na hatimaye mapigano yakasambaa na kusababisha visima vya mafuta kufungwa na kulazimisha theluthi tatu ya idadi ya watu katika nchi kuyakimbia makaazi yao huku wengine 400, 000 wakiuawa.

Mkataba wa amani umesitisha mapigano lakini serikali ya Sudan Kusiniimesema haina fungu la kufadhili uteketezwaji wa silaha na utengamano wa waasi katika jeshi. Pande zote pia hazijakubaliana juu ya yote yaliyomo katika mkataba ikiwemo idadi ya majimbo ambayo Sudan Kusini inatakiwa kuwa nayo. Chini ya makubaliano hayo, Sudan Kusini itafanya uchaguzi mkuu baada ya kipindi cha mpito cha miaka mitatu kumalizika.

Ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliitembelea Juba mapema mwezi huu katika juhudi za kuzishawishi pande zote kutatua masuala yenye utata yaliyosalia katika mkataba. Wachambuzi wanasema kuna uwezekano kwamba mapigano yakarejea upya ikiwa tarehe ya mwisho ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa itapita.