1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la Hamas kwa Israel lazua mjadala Ujerumani

11 Oktoba 2023

Kutokana na mashambulizi ya kundi la Hamas dhidi ya wanajeshi na raia wa Israel, kumekuwa na shinikizo kwa jamii ya Waislamu wanaoishi nchini Ujerumani kujipambanuwa waziwazi upande wanaoegemea kwenye mzozo huu.

https://p.dw.com/p/4XOPP
Bendera ya Ujerumani ikipepea baina ya minara miwili ya msikiti Ujerumani
Bendera ya Ujerumani ikipepea baina ya minara miwili ya msikiti UjerumaniPicha: Stefan Trappe/IMAGO

Kinyume na mara nyengine, safari hii ukosoaji unatoka miongoni mwa baadhi ya Waislamu wenyewe.

Ilianza na ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa X na Waziri wa Chakula na Kilimo wa Ujerumani, Cem Özdemir, aliyeandika,

 "Ukimya mkubwa kutoka kwa jumuiya za Waislamu kuhusiana na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel. Ama maneno yanayolinganisha..... Tunapokabiliana na ugaidi, mauaji na utekaji, kunapaswa hatimaye pawepo na ukomo wa kukosa busara tunaposhughulika na jumuiya za Waislamu." Ujumbe wa Twitter Ulisomeka

Soma pia:Israel inaendelea kufanya mashambulizi dhidi ya ukanda wa Gaza

Mamia ya wanamgambo wa Hamas wenye silaha walivuka mpaka na kuingia Israel kutokea Ukanda wa Gaza mapema ya tarehe 7 Oktoba na kuwauwa na kuwateka nyara wanajeshi na raia wa kawaida.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za serikali ya Israel, ambayo imetangaza vita dhidi ya Gaza, zaidi ya watu 700 waliuawa nchini Israel. 

Kwa upande wake, Israel, ambayo imetangaza kuizingira kikamilifu Gaza, imeshauwa zaidi ya watu 550 hadi sasa ikisema inalipiza kisasi kwenye Ukanda huo.

Muitikio wa jumuiya ya Waislamu Ujerumani

Ukitowa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, na chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto, die Linke, vyama vyote vya siasa kwenye bunge la Ujerumani, Bundestag, vimeonesha mshikamano wao kwa Israel.

Kwenye tamko lao la pamoja, vilisema "Rambirambi zetu kwa watu wa Israel na serikali yao kwenye kipindi hiki kigumu. Lilisema tamko hilo la vyama vya siasa.

Liliongeza kwamba "Hakuna linaloweza kuhalalisha ugaidi kama huu na lazima ukomeshwe haraka."

Hata kabla ya hapo, watu kwenye mtandao wa X walikuwa wametaka jumuiya za Kiislamu nchini Ujerumani kutoa matamko kama hayo.

Waislamu wakiwa katika ibada msikitini
Waislamu wakiwa katika ibada msikitiniPicha: Mesut Zeyrek/AA/picture alliance

Kuna Waislamu wapatao milioni tano unusu wanaoishi maeneo mbalimbali ya Ujerumani.

Soma pia:Upinzani nchini Israel waungana kukabiliana na Hamas

Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa hadi mwaka 2021, kiasi cha asilimia 70 ya misikiti nchini Ujerumani inaratibiwa kwa kiwango cha shirikisho ama ina mahusiano kwenye kiwango cha majimbo.

Michache kati yake iko chini ya uangalizi wa Ofisi ya Ulinzi wa Katiba ya Ujerumani na imekosolewa kwa kupokea fedha kutoka Uturuki na Iran.

Mara tu baada ya ujumbe wa Özdemir, Ali Mete ambaye ni katibu mkuu wa vuguvugu la kidini na kisiasa la jamii ya Waturuki nchini Ujerumani, Milli Gorus, alijibu akiandika,

 "Picha za mashambulizi, utekaji nyara na udhalilishaji ambazo kwa bahati mbaya tumekuwa tukiziona kwa miaka mingi na tunaendelea kuziona leo hazivumiliki. Tunaomba kwamba miongo kadhaa ya mateso kwa Israel na Palestina na pia kwenye maeneo mengine yenye migogoro iishe. Hata hivyo, ni jambo sahihi na ni kutokuwa makini kwa kuwatuhumu Waislamu wa hapa Ujerumani kuhusika na uhalifu ndani ya Israel na Palestina." 

Tamko la Waislamu wa Ujerumani lakosolewa

Ilichukuwa muda mrefu kidogo kwa Baraza Kuu la Waislamu wa Ujerumani, ambalo linaendesha misikiti 300, kutoa tamko lake lililosema kwamba:

"Tunalaani mashambulizi ya hivi karibuni ya Hamas dhidi ya raia na tunataka kukomeshwa ghasia mara moja. Ili kuepuka mabalaa zaidi kwa raia, pande zote zinapaswa kuacha uhasama haraka."

Hata hivyo maneno hayo ya mwisho, yamesababisha ukosoaji mkubwa, huku Baraza hilo likituhumiwa kwa "uhusishaji" ukatili uliofanywa na Hamas.

Israel kuuzingira Ukanda wa Gaza

Miongoni mwa waliokosoa ni Eren Güvercin, mwanzilishi wa jukwaa huru la midahalo ya Waislamu nchini Ujerumani, Alhambra, aliyeandika kupitia mtandao wa X kama ifuatavyo:

"Nikiwa Mjerumani Muislamu, kinachooneshwa hapa na Baraza Kuu la Waislamu ni kitu cha aibu. Hamuwasemei Waislamu wa Ujerumani. Badilisheni jina lenu." 

Danyal Bayaz, waziri wa fedha wa jimbo la Baden-Württemberg kupitia chama cha Walinzi wa Mazingira, Die Grüne, naye pia alionesha hasira zake kwa kusema tamko hilo la Baraza la Waislamu ni njia ya kuonesha mlinganisho tu.

Soma pia:Umoja wa Mataifa waionya Israel juu ya kuizingira Hamas

"Ni tamko la aibu. Mshikamano na Israel hauwezi kuhusishwa na kitu chengine, na hasa baada ya mashambulizi ya kikatili. Mumepotoka."

Aliandika pia kupitia mtandao wa X, zamani ukiitwa Twitter.