1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimetimia siku 500 tangu Urusi ilipoivamia kijeshi Ukraine

Angela Mdungu
8 Julai 2023

Zimetimia siku 500 tangu Urusi ilipoivamia kijeshi Ukraine. Mwisho wa mzozo huu bado hauonekani, huku wanajeshi wa Ukraine wakipata mafanikio kiduchu bila silaha za kutosha.

https://p.dw.com/p/4TcTR
Ukraine Präsident Wolodymyr Selenskyj
Picha: Omar Marques/Getty Images

Katika kuadhimisha siku 500 za uvamizi huo, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, Jumamosi,  amekitembelea kisiwa cha kimkakati cha Snake kilicho katika Bahari Nyeusi ambacho ni alama muhimu ya upinzani wa uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.Amesema ni siku ya kuonesha heshima kwa mashujaa wa Ukraine waliopambania kukikomboa kisiwa hicho ambacho mwanzoni mwa vita, Urusi ilikikamata kabla ya Ukraine kukirejesha kwenye himaya yake mwezi Juni mwaka uliopita. Kupitia ujumbe aloutoa kisiwani hapo, Zelenksy amesema Ukraine kamwe haitadhibitiwa na wavamizi.

Soma zaidi:Zelensky aishukuru Marekani kwa msaada wa kijeshi 

Umoja wa Mataifa umesema unalaani gharama wanayolipa raia wa Ukraine kutokana na mzozo huo. Katika taarifa iliyotolewa na makamu wa mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalofuatilia haki za binadamu Ukraine, HRMMU, Noel Calhoun  zaidi ya raia 9,000 wakiwemo watoto 500 wameuwawa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24. Hata hivyo, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa siku za nyuma waliwahi kusema kwamba idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.

Wakati idadi ya majeruhi kwa mwaka huu ikitajwa kuwa chini kuliko mwaka 2022, idadi hiyo ilianza tena kupanda katika miezi ya Mei na Juni. Itakumbukwa kuwa, Juni 27 raia 13 wakiwemo watoto wanne waliuwawa katika shambulio la kombora huko Kramatorsk, Mashariki mwa Ukraine.

Sehemu ya uharibifu wa vita mjini Lviv, Ukraine
Sehemu ya uharibifu wa vita mjini Lviv, UkrainePicha: STATE EMERGENCY SERVICE OF UKRAINE/REUTERS

Ijumaa, katika mji wa Lviv ulio mbali na uwanja wa mapambano, waokoaji walikuta miili tisa baada watu kufunikwa na vifusi vilivyotokana na kuporomoka kwa majengo baada ya mashambulizi ya Urusi. Karibu watu 37 walijeruhiwa kwenye shambulio la mapema Alhamisi ambalo Meya Andriy Sadovyi, alilitaja kuwa kubwa zaidi kuwahi kufanywa katika miundombinu ya raia tangu vita vilipoanza.

Raia wanazidi kuyakimbia makazi Ukraine, kutokana na mashambulizi

Mji wa Nikopol ulio karibu na uwanja wa mapambano nao umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara na vikosi vya Urusi.  Takriban wakaazi 1,000 wa mji huo wameshaukimbia. Uko karibu na hifadhi ya bwawa la Kakhova, kilometa 10 kutoka katika kinu cha nyuklia cha Zaporhizha  kilicho chini ya udhibiti wa Urusi tangu Machi 2022. Bwawa hilo a Kakhova lililipuliwa, na Ukraine inaishutumu Urusi kwa kitendo hicho inachodai kuwa Urusi ilikifanya kwa makusudi ili kupunguza kasi ya mashambulizi kutoka upande wa Ukraine.

Kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia
Kinu cha nyuklia cha ZaporizhzhiaPicha: Ukrinform

Licha ya kupokea misaada yenye thamani ya mabilioni ya Euro kutoka nchi za Magharibi, jeshi la Urusi limefanikiwa kurejesha vijiji vichache na kilomita chache za mraba za himaya ya Ukraine tangu mapigano yalipoanza.

Hivi sasa Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky, amekuwa akifanya mfululizo wa ziara barani Ulaya akitafuta kuungwa mkono kijeshi hasa kupata silaha bora zaidi kwa ajili ya jeshi lake ambalo lilmeanza kujibu mashambulizi ya Urusi yanayofanyika kwa kasi ndogo kuliko matarajio ya washirika wake. Kwenye ziara hizo, anatafuta pia kuungwa mkono na nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO kabla ya mkutano wa jumuiya hiyo utakaofanyika wiki ijayo.