SIPRI: Mauzo ya silaha ulimwenguni yamepungua kidogo
14 Machi 2022Ripoti ya SIPRI iliyotolewa Jumatatu inaonyesha kuwa ukilinganisha na kipindi cha miaka mitano iliyopita, mauzo ya kimataifa ya silaha kubwa yamepungua kwa asilimia 5 duniani kote. Lakini mauzo ya silaha hizo barani Ulaya yamepanda kwa asilimia 19, ikiwa ndio ongezeko kubwa la kikanda.
Mtafiti wa SIPRI Pieter Wezeman, amesema "Kuzorota kwa uhusiano baina ya mataifa mengi ya Ulaya na Urusi ilikuwa ndio kichocheo kikubwa cha kupanda kwa mauzo ya silaha, hususan kwa mataifa ambayo hayawezi kukidhi mahitaji yake kupitia viwanda vya ndani vya silaha".
Uingereza, Norway na Uholanzi ndio walikuwa waagizaji wakuu barani Ulaya. Uagizaji wa silaha kubwa nchini Ukraine ulikuwa wa kikomo ndani ya kipindi hicho licha ya mvutano na Urusi kuelekea uvamizi wake mwezi uliopita.
Wezeman ameongeza kusema "Mataifa mengine ya Ulaya pia yanatarajiwa kuongeza uagizaji wake wa silaha kwa kiasi kikubwa ndani ya muongo ujao, yakiwa tayari yameagiza silaha hizo haswa ndege za kivita kutoka Marekani".
Marekani imesalia kuwa muuzaji mkuu wa silaha ulimwenguni, ikiwa imeongeza hisa za soko lake hadi asilimia 39 kutoka asilimia 32.
Mauzo ya silaha nzito kama vile vifaru, ndege za kivita na manowari yamepungua kwa asilimia 4.6 ndani ya kipindi hicho. "Kuongeza au kuendelea kwa viwango vya juu vya uagizaji wa silaha kwenye maeneo kama Ulaya, Asia ya Mashariki na Mashariki ya Kati kulichangia wasiwasi wa ushindani wa biashara ya silaha".
Urusi ambayo ilichangia asilimia 19 ya mauzo yote ya silaha kuu kati ya mwaka 2017-2021, ilishuhudia mauzo yake yakishuka kwa asilimia 26 kati ya mwaka 2012 hadi 2016 na 2017-2021. Kwa ujumla kuporomoka kwa mauzo ya silaha nchini Urusi kulitokana na kupungua kwa usambazaji wa silaha kwa wateja wawili ambao ni India na Vietnam.
Licha ya kupungua kwa mauzo, Ujerumani imesalia kuwa miongoni mwa mataifa matano makubwa ya wauzaji wa silaha. Mauzo ya Ujerumani yalishuka kwa asilimia 19 kati ya mwaka 2012-2016 na 2017-2021, imesema ripoti hiyo.
Data za SIPRI hutegemea taarifa na makadirio ya usafirishaji wa kimataifa wa silaha ikiwa ni pamoja na mauzo, zawadi na uzalishaji chini ya leseni na hutathmini wingi wa usambazaji huo na sio thamani ya fedha ya mikataba.
Vyanzo: reuters/dpa