1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Somalia kujadili makubaliano ya Somaliland na Ethiopia

2 Januari 2024

Somalia itafanya mkutano wa dharura wa baraza lake la mawaziri leo baada ya jimbo lililojitenga la Somaliland kufikia makubaliano yenye utata na Ethiopia na kuipa nchi hiyo nafasi ya kuifikia Bahari ya Shamu.

https://p.dw.com/p/4an6z
Mji wa bandari wa Berbera
Berbera ni mji wa bandari kaskazini mwa Somalia kwenye Ghuba ya Aden, katika jimbo la Somaliland linalojitawala lakini halitambuliki kimataifa.Picha: Yannick Tylle/picture alliance

Somalia itafanya mkutano wa dharura wa baraza lake la mawaziri leo baada ya jimbo lililojitenga la Somaliland kufikia makubaliano yenye utata na Ethiopia na kuipa nchi hiyo nafasi ya kuifikia Bahari ya Shamu.

Makubaliano hayo ya kushtukiza kati ya Ethiopia na Somaliland yamezua ghadhabu mjini Mogadishu, ambayo inayachukulia kama ukiukaji wa uhuru wake.

Makubaliano hayo yametangazwa siku chache tu baada ya serikali kuu ya Somalia kuanza tena mazungumzo na Somaliland baada ya miaka mingi ya mkwamo.

soma pia: Utawala wa Somaliland umesema hauna mpango wa kujiunga tena na Somalia

Kwa makubaliano hayo, Ethiopia ambayo haina mpaka wa bahari, inapata fursa ya moja kwa moja kuitumia Bahari ya Sham kama njia ya biashara za kimataifa.

Somaliland imekuwa ikitaka kutambuliwa kimataifa kama taifa huru tangu ilipojiengua kutoka Somalia mnamo mwaka 1991, hatua inayopingwa vikali na Mogadishu.