Sri Lanka yapiga kura katika uchaguzi wa mapema wa bunge
14 Novemba 2024Sri Lanka inapiga kura leo katika uchaguzi wa pili wa kitaifa wa bunge huku upinzani uliogawanyika ukitafuta kujikwamua kutokana na kushindwa vibaya katika uchaguzi wa urais.
Uchaguzi wa mapema wa ubunge uliitishwa na Rais mpya Anura Kumara Dissanayake, kiongozi wa kwanza wa mrengo wa kushoto katika taifa hilo la Asia Kusini, baada ya kushinda kura kwa ahadi ya kupambana na ufisadi na kurejesha mali zilizoibwa nchini humo.
Chama chake kinapewa nafasi kubwa ya kushinda viti vingi katika uchaguzi wa leo huku wachambuzi wakisema upinzani uko katika mkanganyiko.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 55 anatafuta kura ya theluthi mbili katika bunge lenye wabunge 225 ili kuendeleza mageuzi baada ya kuzorota kwa uchumi wa nchi hiyo mwaka 2022, wakati rais wa wakati huo Gotabaya Rajapaksa alipoondolewa madarakani.