Sudan Kusini kufunga shule zote kutokana na joto kali
18 Machi 2024Wizara za afya na elimu nchini humo zimewashauri wazazi kutowaruhusu watoto wao kutoka nje katika wakati ambapo viwango vya joto vinatarajiwa kuongezeka hadi nyuzi joto 45.
Shule zitakazokaidi amri ya kufungwa zitapokonywa leseni za usajili
Katika taarifa iliotolewa Jumamosi jioni, wizara hizo zimeonya kuwa shule yoyote itakayopatikana imefunguliwa wakati wa kipindi hicho cha tahadhari, itapokonywa leseni yake ya usajili lakini hazikufafanua muda wa kufungwa kwa shule hizo.
Joto kali laripotiwa kusababisha vifo
Pia zimesema kuwa tayari kunaripotiwa vifo vinavyotokana na joto hilo kali bila ya kutoa maelezo zaidi.
Wizara hizo zimeshauri kufuatiliwa kwa watoto wadogo kwa dalili zozote za magonjwa yanayotokana na joto kali na kuongeza kuwa zitaendelea kufuatilia hali hiyo na kutoa taarifa mwafaka kwa umma.
Shule zinapaswa kuwa na viyoyozi
Peter Garang, mkazi wa mji mkuu wa nchi hiyo, Juba, amepongeza uamuzi huo na kusema kuwa shule zinapaswa kuunganishwa katika gridi ya umeme kuwezesha kuwekwa kwa viyoyozi.
Sudan Kusini, moja ya mataifa changa duniani, mara kwa mara huathirika kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na vipindi vya joto kali ambavyo ni nadra kuzidi viwango vya nyuzi joto 40.
Vipindi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea nchini Sudan Kusini
Wanasayansi wanasema mawimbi ya joto kali ya mara kwa mara ni kiashiria cha wazi cha ongezeko la joto duniani na kuongeza kwamba mawimbi hayo yanatarajiwa kuendelea kutokea mara kwa mara na kwa vipindi virefu.
Sudan Kusini imeathirika kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe
Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yameikumba nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambayo pia iliathirika kutokana na ukame na mafuriko na kufanya hali ya maisha kuwa ngumu kwa wakazi.
WFP yasema mzozo wa kibinadamu umekithiri Sudan Kusini
Ripoti ya karibuni zaidi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula- WFP kuhusu taifa hilo laSudan Kusini,inasema kuwa nchi hiyo inaendelea kukabiliwa na mzozo mbaya wa kibinadamu kutokana na migogoro, kuyumba kwa uchumi na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wanaokimbia mapigano kutoka taifa jirani la Sudan.
Soma pia:Hali inazidi kuwa mbaya Sudan Kusini
WFP imeongeza kuwa mwezi Januari, watu 818,000 wanaoishi katika mazingira magumu, walipewa msaada wa chakula na pesa .