Sudan Kusini yakabiliwa na janga la njaa
17 Aprili 2014Onyo hilo limetolewa na katibu mkuu wa umoja huo Ban Ki-Moon wakati ambapo hali ikizidi kuwa ya kuogofya, na serikali ikikiri kuupoteza mji muhimu wa Bentiu kwa waasi.
Katibu mkuu Ban alisema siku ya Jumatano kuwa taifa hilo changa kabisaa duniani linakabiliwa na masuala ya kufa na kupona, yakiwemo mapigano, utapiamlo na hali mbaya ya kibinaadamu.
Alisema mamilioni wanashinda na njaa leo, na kwamba Umoja wa Mataifa unashuhudia viwango vikubwa vya utapiamlo miongoni mwa mamia ya watu waliogeuzwa wakimbizi na mgogoro huo, hususani wanawake na watoto.
Sudan Kusini imekumbwa na mgogoro tangu mwezi Desemba mwaka jana, baada ya kuibuka mapigano kati ya wanajeshi watiifu kwa makamu wa zamani wa rais aliendolewa Riek Machar na wale wanaomtii rais Salva kiir.
'Mwanzo wa ukombozi'
Waasi walisema Jumatano kuwa waliuteka mji wa mkuu wa Bentiu, katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Unity, na wameyaonya makampuni ya mafuta kufungasha virago vyao na kuondoka ndani ya wiki moja.
Msemaji wa waasi Lul Ruai Koang alisema kutekwa kwa mji wa Bentiu ndiyo mwanzo wa ukombozi wa visima vya mafuta kutoka kwa vikosi vya mauaji na visivyo vya kidemokrasia vya rais Salva Kiir.
"Ikiwa unataka kumuondoa dikteta, mji wa Juba na visima vya mafuta ndiyo shabaha. Ananunua silaha zaidi, na anafanya vitendo zaidi vya rushwa kwa kutumia rasilimali zetu," alisema Machar siku ya Jumatatu,kabla ya vurugu kuukumba mji wa Bentiu
Maelfu wanaaminika kuuawa na zaidi ya milioni moja wameyakimbia makaazi yao. Makundi ya misaada ya kibinaadamu yanasema yanakimbizana na muda kuweza kuzuwia janga la njaa. Jeshi la Sudan Kusini lilikiri jana kuwa waasi wamewanyanganya mji wa Bentiu, huku msemaji wa jeshi hilo Philip Aguer, akiwalaum wanamgambo wa kabila la Misseryia kutoka nje ya mipaka ya Sudan Kusini kwa kumsaidia Machar.
Kitisho cha kuwekewa vikwazo
Katibu mkuu Ban alisema ujumbe wa umoja uko bayana - tunahitaji kusitishwa kwa mapigano, kupatikana kwa suluhisho la kisiasa kwa mgogoro huo na tunahitaji kuwezeshwa ili tuendelee kutoa msaada wa kuokoa maisha.
Umoja wa Mataifa unatoa hifadhi ya moja kwa moja kwa Wasudan Kusini zaidi ya 85,000, ambao wamechukuwa hifadhi katika vituo vyake vilivyoko nchini kote.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotiwa saini mwezi Januari yamevinjwa mara kwa mara, na mazungumzo ya mjini Adis Ababa yamekuwa yakikwama kila mara. Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya na Norway zimetishia kuyawekea vikwazo makundi hasimu.
Mwezi uliyopita, rais Barack Obama aliidhinisha uwezekano wa vikwazo dhidi ya wale wanaofanya uhalifu dhidi ya binaadamu, au wanaodhoofisha demokrasia na kukwamisha mchakato wa amani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,dpae,ape
Mhariri: Sudi Mnette