Sudan Kusini yakanusha kushindwa kwenye vita vya Heglig
21 Aprili 2012Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki- Moon, amezitaka pande mbili zinazozozana kurejea katika njia ya mazungumzo kama suluhu wakati huu ambapo kituo cha walinda amani wa Umoja huo nchini Sudan kimeshambuliwa siku kadhaa zilizopita.
Lakini tofauti za mitazamo kuhusu hatma ya mji huo wenye mafuta ambao vikosi vya Sudani ya Kusini viliingia siku kumi zilizopita zinazidi kuchukua nafasi kubwa miongoni mwa pande hizo mbili.
Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Daffa Alla Elhag Ali Osman, amesema kuwa vikosi vya Sudan ya Kusini vimefukuzwa. "Wamezungukwa, tumepigana nao na tukawafukuza. Si kwamba wamejiondoa, tumewafukuza," alisema balozi huyo kuwaambia waandishi wa habari.
"Hatukuondoshwa, tuliondoka wenyewe"
Wakati hayo yakijiri upande wa Sudan, naye Balozi wa Sudan ya Kusini katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa vikosi vya nchi hiyo vinaendelea kuondoka katika eneo hilo. "Zoezi la kuondoa vikosi vya Sudan Kusini katika mji wa Heglig litakamilika katika siku tatu zijazo", alisema Balozi Agnes Oswaha akithibitisha kauli ya rais wa nchi yake, Salva Kiir. Alisema waandishi wa habari na waangalizi wa kimataifa wanakaribishwa Heglig kujionea nani mwenye mamlaka ya mji huo.
Osman anasema kuwa Sudan haitakiuka mipaka ya kimaifa iliyowekwa baina ya nchi hizo mbili. Wanatumai kuwa Sudan Kusini imejifunza na haitarudia tena kufanya kitendo cha uvamizi kama walichofanya kwa Heglig.
Sudan inasema kuwa serikali ya Sudan Kusini ni tofauti na watu wa nchi hiyo. Watawala wanafaya mambo kama vie wana akili za nyani, kwa sababu walikuwa viongozi wa makundi ya waasi na hata sasa wamepata uongozi bado akili ya kisokwe wanayo, alisema balozi Osman.
"Heglig itakuwa ya Sudan ya Kusini"
Sudan ya Kusini ilijitenga na Kaskazini baada ya kura ya maoni iliyopigwa kufuatia makubaliano ya amani ya mwaka 2005 yaliyositisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miongo miwili ambapo zaid ya watu milioni waliuawa.
Balozi huyo wa Sudan ya Kusini amesem kuwa mji wa Heglig ambao nchi hiyo inauita kwa jina la Panthou, utaendedelea kubakia eneo lake na kwamba mgogoro uliopo lazima utatuliwe na na jumuiya za usluhishi za kimataifa pamoja na maeneo mengine yaliyo katika mzozo kwenye eneo la mpakani.
Vita vinaweza kutokea tena kama hatua za haraka za kutatua mzozo huu haizachukuliwa na Jumiya za Kimataifa.
Kwa mujibu wa Balozi Oswaha, Sudan Kusini imeondoa vikosi vyake Heglig kwa kuwa haitaki kuingia tena katika mapigano na inatafuta njia ya haraka na ya amani ya kutatua mzozo huo.
Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Eduardo del Buey, amesema kuwa wanatilia maanani ahadi ya kusini kujiondoa katika mji wa Heglig. Aidha, Katibu Mkuu, Ki-moon, amesisitiza pande zinazozozana kurejea katika meza ya mazungumzo ili kupata suluhu kupitia mjumbe wa Umoja wa Afrika katika mzozo huo Thabo Mbeki.
Mwandishi: Stumai George
Mhariri: Mohammed Khelef