Susan Rice mshauri wa usalama wa taifa
6 Juni 2013Licha ya shutuma kuwa alitoa taarifa zisizo sahihi kwa taifa baada ya mashambulio mabaya dhidi ya raia wa Marekani mjini Benghazi, nchini Libya Rice anachukua wadhifa huo kutoka kwa mshauri anayeondoka madarakani Tom Donilon.
Uteuzi huo uliofanywa jana Jumatano(05.06.2013) , pamoja na uteuzi wa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu Samantha Power kuchukua nafasi inayoachwa wazi na Rice kama balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa , unaashiria hatua ya Obama kuwapendelea washauri ambao wana mwelekeo wa kupendelea uingiliaji kati zaidi wa Marekani nchi za nje kwa minajili ya kuchukua hatua za kibinadamu.
Obama hatarajiwi kubadilika
Lakini bado si wazi iwapo nadharia hiyo itabadilisha sera za rais Obama kuhusu Syria , ambako amezuwia mbinyo hadi sasa wa kutumia nguvu za kijeshi kuutatua mzozo wa nchi hiyo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Uteuzi wa Rice unatoa unatoa nafasi ya kupumua kidogo baada ya uchunguzi wenye utata uliofanyika mjini Benghazi kulazimisha kutoweza kufikiriwa kuchukua wadhifa wa waziri wa mambo ya kigeni katika kipindi cha pili cha utawala wa Obama .
Rais , ambaye alimtetea Rice kwa nguvu zote dhidi ya ukosoaji kutoka kwa wabunge wa chama cha Republican , amemsifu rafiki yake huyo wa karibu kwa kusema kuwa ni mzalendo halisi ambaye huweka maslahi ya nchi yake kwanza.
Wasifu
"Susan ni mtumishi halisi wa umma, ambaye huweka maslahi ya nchi yake mbele. Simuwoga na ni jasiri. Susan anatambua kuwa hakuna kitu mbadala kwa uongozi wa Marekani. Ni mwenye hamasa , na mtendaji. Na natambua kuwa Susan ni bingwa wa kweli wa kupigania haki na ubinadamu."
Lakini pia ni mtu mwenye kutambua kuwa tunapaswa kutumia nguvu zetu kwa busara na panapostahili.
Rice mwenye umri wa miaka 48 anachukua wadhifa huo wenye ushawishi mkubwa wa usalama wa taifa akiwa mtu wa karibu kabisa na rais kutoka kwa Tom Donilon , ambaye anaacha wadhifa huo mwezi Julai baada ya kutumikia kwa muda wa zaidi ya miaka mitano katika utawala wa rais Obamna.
Mabadiliko katika ngazi ya juu ya kikosi cha utawala cha rais Obama yanakuja muda mfupi wakati akianza kupambana na agenda ya sera za mambo ya kigeni. Anatarajiwa kukutana na rais wa China Xi Jinping katika mkutano usio wa kawaida mjini Califonia kuanzia Ijumaa, na kisha atasafiri kwenda katika mataifa ya Ulaya na Afrika baadaye mwezi huu.
Mwandishi: Sekione Kitojo/ape
Mhariri: Mohammed Khelef