1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yakubali kukaguliwa, Marekani yasema imechelewa

26 Agosti 2013

Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wameanza kuchunguza madai ya matumizi ya silaha za kemikali karibu na mji wa Damascus wiki iliyopita, huku Marekani ikisema hatua ya Syria ya kukubali uchunguzi huo imekuja kuchelewa.

https://p.dw.com/p/19W27
epa03836543 A handout photo made available by the Syrian Arab News Agency (SANA) shows Syrian President Bashar Assad (C) meeting with newly-appointed ministers in Damascus, Syria, 25 August 2013. Assad on 22 August appointed six new ministers for higher education, economy, industry, internal trade, tourism, and a state minister. The new ministers were sworn-in on 25 August before meeting with Assad. EPA/SANA/HANDOUT HANDOUT EDITORIAL USE ONLY/NO SALES
Syrien Präsident Assad mit neuen MinisternPicha: picture-alliance/dpa

Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wameanza kuchunguzi matumizi ya silaha za kemikali katika eneo lililoshambuliwa karibu na mji wa Damascus wiki iliyopita, huku Marekani ikisema hatua ya Syria ya kukubali uchunguzi huo imekuja kuchelewa.

Hatua ya kuruhusiwa wakaguzi hao kulikagua eneo yalikofanyika mashambulizi hayo ilifuatia tangazo lililotolewa na wizara ya mambo ya kigeni kupitia televisheni ya taifa ya Syria, kwamba makubaliano yalikuwa yamefikiwa na mkuu wa kitengo cha kupunguza matumizi ya silaha cha Umoja wa Mataifa Angela Kane. Lakini maafisa wa Marekani wamesema hatua hiyo imechelewa sana, na kuongeza kuwa mashambulizi ya mfululizo dhidi ya eneo hilo katika siku za hivi karibuni, yameharibu ushahidi.

Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-Muallem katika mkutano wa mkuu wa kitengo cha kupunguza matumizi ya silaha cha Umoja wa Mataifa, Angela Kane.
Waziri wa mambo ya nje wa Syria Walid al-Muallem katika mkutano wa mkuu wa kitengo cha kupunguza matumizi ya silaha cha Umoja wa Mataifa, Angela Kane.Picha: Reuters

Marekani na washirika wake wameinyooshea kidole serikali ya rais Bashar al-Assad kwa kuhusika na shambulizi hilo japokuwa utawala mjini Damascus unakanusha vikali na unawalaumu waasi, huku mshirika wa utawala huo, Urusi nayo ikisema ina ushahidi kuwa waasi ndiyo walifanya shambulizi hilo. Afisa mmoja mjini Washington, alisema kuwa hakuna shaka kuwa silaha za kemikali zilitumiwa na utawala wa Assad dhidi ya raia wake.

Hatua zaweza kuchukuliwa bila idhini ya baraza la usalama

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel alisema ikulu ya White House iko tayari kwa lolote. "Rais Obama ameiomba wizara ya ulinzi kujiandaa na uwezekano wote. Tumefanya hivyo. Tena tuko tayari kutumia njia yoyote, ikiwa rais ataamua kutumia mojawapo ya njia zilizopo," alisema waziri Hagel.

Rais wa Ufaransa Francoise Hollande alimuambia rais Obama kuwa kila kitu kinaonyesha kuwa utawala mjini Damascus ulikuwa nyuma ya shambulizi hilo. Marais hao wawili walikubaliana kuendela kuwasiliana ili kufikia makubaliano kuhusu hatua ya pamoja dhidi ya utawala wa Assad.

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza William Hague, alisema serikali ya Syria haiwezi kukwepa kuadhibiwa, na kuongeza kuwa hatua zinaweza kuchukuliwa pasipo uungwaji mkono wa Umoja wa Mataifa, na kusisitiza kuwa, "hatuwezi katika karne hii ya 21 kuruhusu dhana kwamba silaha za kemikali zinaweza kutumika bila kuchukuliwa hatua, na kwamba watu wanaweza kuuawa kwa namna hii na kusiwepo madhara kwa hilo."

Hata hivyo, waziri mkuu wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault aliashiria kuwa shambulizi dhidi ya Syria si jambo lililoko katika mipango ya haraka. "Baada ya kukamilika kwa uchunguzi huu wa Umoja wa Mataifa, tunasubiri uamuzi wa uhakika, uamuzi bayana kutoka kwa jamii ya kimataifa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana," Ayrault aliiambia Televisheni ya France 2 katika mahojiano.

Urusi yaonya juu ya madhara makubwa

Shirika la habari la serikali ya Syria SANA lilisema kuwa waziri wa habari Omran Zoabi, ameonya kuwa hatua ya kijeshi ya Marekani itasababisha madhara makubwa na kuwasha mtoto utaoizingira kanda nzima ya mashariki ya kati. Urusi ilikaribisha hatua ya Syria kuwaruhusu wakaguzi mjini Damascus, lakini ilionya kuwa hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo itakuwa na madhara makubwa. Rais Assad mwenyewe alisema katika mahojiano na gazeti la Urusi, kuwa madai ya matumizi ya silaha za kemikali ni matusi kwa akili ya kawaida, na kuionya Marekani kuwa itashindwa vibaya itakapojaribu kuishambulia kijeshi Syria.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon aliwambia waandishi wa habari mjini Seoul leo, wakati akihitimisha ziara ya siku tano, kuwa hakuna tena muda wa kupoteza, na kutaka wakaguzi waruhusiwe kutembelea maeneo yote husika pasipo vizuizi vyovyote. Ban alisema mafanikio ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ni katika maslahi ya kila mtu, na yatasaidia kuzuiwa matumizi ya silaha za kemikali katika siku zijazo.

Njiwa wakiwa wamekufa kutokana na kile wanaharakati walichosema ni matumizi ya silaha za kemikali na vikosi vitiifu kwa rais Bashar al-Assad.
Njiwa wakiwa wamekufa kutokana na kile wanaharakati walichosema ni matumizi ya silaha za kemikali na vikosi vitiifu kwa rais Bashar al-Assad.Picha: Reuters

Ni shambulio litakalobadilisha mwelekeo wa vita vya Syria?
Upinzani wa Syria unasema zaidi ya watu 1,300 waliuawa wakati vikosi vya utawala wa Assad vilipotumia silaha za kemikali dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na waasi mashariki na magharibi mwa mji mkuu Damascus Jumatano wiki iliyopita, wakati shirika la madaktari wasio na mipaka lilisema watu 355 walikufa kutokana na dalili za kuvuta hewa ya sumu.

Damascus imekanusha kwa ngvu zote kuwa ilifanya shambulizi hilo, na badala yake imewalaumu waasi. Huku ngoma za vita vikubwa zikipigwa, mshirika wa Syria, Urusi imetoa onya kali kwa nchi za magharibi, kuwa hatua za kijeshi dhidi ya utawala wa Assad litakuwa kosa la maafa.

Maafisa wa Marekani wanakutana na maafisa wa kijeshi kutoka mataifa ya Ulaya na Mashariki ya Kati Jumatatu hii nchini Jordan, katika mkutano ambao ulipangwa kufanyika kabla ya shambulio la wiki iliyopita, lakini ambalo bila shaka litakuwa la kipaumbele katika ajenda ya mkutano huo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe, rtre, Ap
Mhariri: Josephat Charo