Taiwan yamtaka Scholz aionye China isiivamie kijeshi
12 Aprili 2024Hayo yamesemwa na muwakilishi wa kisiwa hicho nchini Ujerumani Shieh Jhy-Weys aliyeongeza kuwa Scholz tayari alishapata maneno sahihi ya kulizungumzia suala hilo katika ziara yake iliyotangulia ya mwezi Novemba mwaka 2022.
Katika mahojiano na shirika la habari la Ujerumani la dpa, muwakilishi huyo wa Taiwan nchini Ujerumani amesema kuwa, licha ya kuwa Kansela Olaf Scholz alilizungumzia suala hilo katika ziara yake iliyopita ya huko China, bado vitisho dhidi ya kisiwa hicho vimekuwa vikiongezeka tangu wakati huo. Ameongeza kuwa huenda China haikuelewa ujumbe huo hivyo haitokuwa jambo baya kwa Kansela Scholz kuurudia tena kinagaubaga ujumbe wake atakapokwenda tena katika ziara yake ya siku tatu inayoanza kesho Jumamosi.
Soma zaidi: Ujerumani kuimarisha uhusiano na Taiwan baada ya uchaguzi nchini humo
Muwakilishi huyo wa Taiwan nchini Ujerumani amebainisha kuwa uvamizi unaoweza kufanywa na China unaweza kuathiri maslahi ya Ujerumani pamoja na Umoja wa Ulaya. Ameongeza kuwa kwa kuwa uchumi wa Ujerumani na Ulaya unategemea baadhi ya vipuri vya kutengenezea bidhaa kutoka Taiwan, hilo inaweza kutumiwa na China kama "Silaha ya kiuchumi na teknolojia." Katika mahojiano hayo Shieh amemhimiza Scholz kuendelea kutafuta njia ya kupunguza utegemezi wa kiuchumi kwa China.
Kansela Scholz kuambatana na mawaziri na wafanyabiashara
Katika ziara ya siku tatu, kiongozi huyo wa Ujerumani atakutana na Rais Xi Jinping, na wawakilishi wengine wa serikali ya China. Ataambatana na mawaziri wake watatu sambamba na wafanyabiashara. Taiwan imekuwa na serikali huru tangu mwaka 1949 lakini serikali ya Jamhuri ya watu wa China inakichukulia kisiwa hicho chenye wakaazi milioni 23 kuwa sehemu ya himaya yake.
China pia, imekuwa ikikataa kuwepo kwa mawasiliano yoyote rasmi ya kidiplomasia kati ya Taiwan na mataifa mengine ulimwenguni. Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, kumekuwa na hofu inayoendelea kuongezeka kuwa huenda China nayo ikaivamia Taiwan. Sababu nyingine ya hofu hiyo inatokana na serikali ya China kutishia mara kwa mara kuwa itakitwaa kisiwa hicho kwa mabavu.
Muwakilishi wa Taiwan nchini Ujerumani Bwana Shieh Jhy-Weys ameitaka Ujerumani kupeleka wanajeshi wake katika mlango bahari ulio kati ya Taiwan na China kama zilivyofanya Marekani, Uingereza na Ufaransa. Mwezi Mei, meli ya kivita na nyingine itakayobeba mahitaji mengine zitaelekea Pasifiki kulinda maslahi ya Ujerumani katika ukanda huo pamoja na njia zake muhimu za kibiashara.
Ujumbe kama huo tayari ulishapelekwa kati ya mwezi Agosti mwaka 2021 na Februari 2022. Shieh amesema kuwa anatumaini kwamba Ujerumani itafanya kazi kwa ukaribu zaidi na Taiwan.