Tanzania na mkakati wake wa kushughulikia corona
11 Machi 2021Hadi wakati huu ni vigumu kutambua moja kwa moja kama Tanzania inaandamwa na maambukizi ya virusi vya corona au la, ingawa kumekuwa na ripoti zinazoashiria kwamba taifa hili ni miongoni mwa mataifa ambayo yamepata pigo kutokana na janga hilo la kidunia.
Takwimu za serikali hazionyeshi moja kwa moja kama maambukizi hayo yamekuwa yakipanda, kutokuwepo kabisa au yamepungua na mara ya mwisho wizara ya afya kutangaza takwimu za wagonjwa COVID-19 ilikuwa Aprili mwaka 2020.
Kwa ujumla wakati leo inatimia mwaka mmoja tangu shirika la afya duniani WHO, ilipojitokeza na kulitaja tatizo la maambukizi ya virusi vya corona ni janga la dunia, Tanzania imeandika ramani ya kipekee kwa jinsi ilivyokabiliana na janga hili na hadi wakati huu kunapotajwa kujitokeza kile kinachosemwa wimbi jipya la maambukizi hayo bado taifa hili halijabadili mwenendo wake.
Matumizi ya imani yaani ibada ya kuomba huruma ya Mwenyezi Mungu, kuwepo kampeni kubwa inayohimiza utumiaji wa njia za asili kama vile kufukiza na mambo mengine yanayohusiana na hali hiyo, ni moja ya ngao inayoelezwa kwamba ndiyo inayofanya Tanzania ijivunie kuushinda ugonjwa huo.
Rais John Magufuli ambaye tangu kuibuka kwa janga hilo, amekuwa akijitokeza hadharani kuwataka wananchi kutokuwa na hofu, mara kwa mara amekuwa akisema jinsi Tanzania ilivyokabiliana na maambukizi hayo na hatimaye kuyashinda.
Soma pia: Tanzania: Serikali zingatieni utaalamu kwenye chanjo
Ingawa hivi karibuni alikiri juu ya kurejea tena kwa maambukizi hayo, hata hivyo hajapindisha msimamo wake kuhusu kuendelea kumtegea Mungu katika vita hii.
Wakati huu ambako dunia inahubiri jambo moja kuhusu kuwapa chanjo raia wake ili kukabiliana na maambukizi hayo, bado Tanzania inajitokeza tena kwenye ramani ya dunia kwa namna isivyokubaliana na utoaji wa chanjo hiyo.
Licha ya mataifa mengi jirani kuingia katika mpango wa utoaji chanjo kupitia mradi wa kimataifa kwa ajili ya kuzisaidia nchi maskini ujulikanao kama Covax, Serikali ya Tanzania imesema haiko tayari kupokea chanjo hiyo, na ni majuzi tu, Msemaji wa Serikali Dk Hassan Abbas aliwaambia waandishi wahabari, kuhusu Tanzania kutounga mkono chanjo hizo.
Ingawa Tanzania inasisitiza kuchukua mkondo wa aina yake katika kukabiliana na janga hilo, hata hivyo imekuwa ikiandamwa na shutuma kali kutoka ndani na nje ya nchi hasa wakati huu kunapotajwa kujitokeza kwa wimbi jipya la maambukizi.
Wito huu umepata msukumo mpya katika siku za hivi karibuni kutoka kwa makundi mbalimbali hasa baada ya ripoti kuonyesha kuwepo kwa ongezeko kubwa la watu wanaopoteza maisha kutokana na kile kinachoelezwa ni matatizo ya upumiaji.