Theresa May athibitisha kujiuzulu
24 Mei 2019Hii ini baada ya kushindwa kupata uungwaji mkono wa wabunge katika mpango wake wa kujiondoa kutoka kwenye Umoja wa Ulaya, Brexit.
"Nitaiacha kazi hii karibuni na imekuwa ni fahari kubwa kuishikilia nafasi ya Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke na bila shaka si wa mwisho. Naondoka bila nia mbaya ila shukrani kubwa ya kuweza kuihudumia nchi ninayoipenda," alisema May.
Waziri Mkuu huyo lakini ataikaimu nafasi hiyo ya kiongozi wa chama cha Kihafidhina hadi pale kiongozi mpya atakapochaguliwa hatua ambayo inatarajiwa kuchukua wiki kadhaa. Baada ya hapo kiongozi huyo mpya atachukua nafasi ya Waziri Mkuu na hakutakuwa na haja ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
May hajayatimiza malengo aliyokuwa nayo wakati anachukua uongozi
Mbunge yeyote wa chama cha Kihafidhina anaweza kuiwania nafasi hiyo ya uongozi wa chama, lakini mtu anayepewa nafasi wa kwanza kwa sasa ni Boris Johnson, ambaye ni waziri wa mambo ya nje wa zamani na shabiki mkubwa wa Brexit.
May anaachia ngazi akiwa hajayatimiza malengo aliyokuwa ameapa kuyatimiza wakati alipokuwa anachukua nafasi hiyo ya waziri mkuu. Wakati huo alisema kuwa angelihakikisha kuwa Uingereza imejiondoa kutoka Umoja wa Ulaya na atapatanisha pande zilizogawika kutokana na suala hilo la Brexit.
Kuondoka kwake kutauzidisha mzozo wa Brexit kwa kuwa kuna uwezekano kwamba kiongozi mpya atataka makubaliano mazuri zaidi ya kujiondoa jambo ambalo litazua mkwaruzano na Umoja wa Ulaya na hata uchaguzi wa mapema wa bunge. Umoja wa Ulaya tayari umesema kuwa hautafanya majadiliano mengine zaidi kuhusiana na maelewano waliyoafikiana na May mwezi Novemba.
Shinikizo lilikuwa linazidi kadri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga
Waziri Mkuu huyo anaondoka afisini akiwa ameiacha Uingereza ikiwa imegawika pakubwa na wanasiasa ambao hawajui ni kwa njia gani, lini au hata iwapo waifanikishe hiyo talaka yao na Umoja wa Ulaya.
Shinikizo lilikuwa kubwa zaidi kutoka kwa chama chake baada ya kushindwa kuiongoza Uingereza katika Brexit katika muda uliokuwa umepangiwa. Mamlaka yake yalikuwa yanaonekana kupungua kadri muda ulivyokuwa ukisonga na Alhamis May alichelewesha kuwasilisha mswada wake wa Brexit, jambo ambalo lingekuwa jaribio lake la nne kutaka kupata idhini ya bunge kuhusiana na makubaliano yake na Umoja wa Ulaya.
Uingereza inatarajiwa kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya Oktoba 31 lakini hilo litafanyika iwapo tu bunge litaidhinisha maelewano ya talaka hiyo.