Trump aanza ziara rasmi nchini Uingereza
3 Juni 2019Rais Trump na mkewe Melania waliwasili mapema leo asubuhi katika uwanja wa ndege wa Stansted na kulakiwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Jeremy Hunt, Balozi wa Marekani nchini Uingereza, Woody Johnson, na maafisa wengine wa serikali.
Malkia wa Uingereza Elizabeth wa II anatarajiwa kuwakaribisha Trump na mkewe katika kasri la Buckingham kwa heshima zote za kijeshi na zulia jekundu, mapokezi yatakayofuatiwa na chakula cha mchana, kabla ya baadaye kutashiriki dhifa ya kitaifa.
Ajenda kuu ya ziara ya Trump nchini Uingereza ni kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili ambayo itajumuisha mikutano kadhaa na Malkia Elizabeth, kuhudhuria kumbukumbu ya miaka 75 ya tukio muhimu la wakati wa vita kuu ya pili ya dunia pamoja na ziara ya kwanza rasmi huko Ireland ambayo ni sehemu ya Uingereza.
Kadhalika rais Trump amepangiwa kukutana na waziri mkuu anayeondoka Theresa May ambapo wawili hao watasisitiza umuhimu wa uhusiano kati ya Londn na Washington.
Trump amshambulia Meya wa London
Lakini Trump ameanza ziara yake kwa kumshambulia meya wa mji wa London, Sadiq Khan, ambaye alisema Uingereza haikupaswa kumkaribisha kiongozi huyo wa Marekani.
Muda mfupi kabla ya kuwasili, Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa meya wa London ni mwanasiasa aliyeshindwa vibaya katika majukumu yake na kwamba anapaswa kushughulikia changamoto ya uhalifu kwenye mji wa London badala ya kujadili ziara yake.
Kwenye makala ya Khan iliyochapishwa na gazeti moja jana Jumapili, meya huyo wa London alisema Trump ni moja ya mifano ya kitisho kinachoongezeka duniani kutoka wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia.
Wale wanamuunga mkono meya huyo wa London wameyaita matamshi ya Trump kuwa ya kibaguzi dhidi ya Khan ambaye ni meya wa kwanza Muislam wa mji huo mkuu.
Kiwingu kwenye ziara ya Trump
Ziara ya Trump inafanyika siku chache tangu alipotoa matamshi yaliyoashiria kuingilia siasa za Uingereza aliposema anaamini kuwa Boris Johnson anafaa kuwa waziri mkuu ajaye wakati May atakapojiuzulu Ijumaa hii.
Wakati wa mahojiano na gazeti la Sunday Times, Trump alisema huenda akakutana na Boris Johnson pamoja na mwanasiasa anayeunga mkono mchakato wa Uingereza kujiondoa kutoka Umoja wa Ulaya, Nigel Farage.
Wanasiasa wa upinzani wamesema watasusia dhifa ya kitaifa na maandamano makubwa kupinga ziara ya Trump yanatarajiwa kufanyika mjini London.
Mahusiano kati ya Marekani na Uingereza yameingia doa katika miaka ya karibuni kutokana na tofauti za kisera katika kushughulikia masuala muhimu ikiwemo suala la Iran, China na mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi wa mjini Paris.