1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump aenda New York kuyakabili mashtaka dhidi yake

3 Aprili 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kwenda New York hii leo kwa ajili ya kusikiliza kesi ya uhalifu inayomkabili kufatia madai ya kumlipa fedha mcheza filamu za ngono kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016.

https://p.dw.com/p/4PckZ
USA | Ex-Präsident Donald Trump bei der NCAA Wrestling Championships
Picha: Sue Ogrock/AP/dpa/picture alliance

Wafuatiliaji wa mambo wanaiona hatua hii kama inayoitia doa na kuibua sintofahamu kubwa juu ya mustakabali wa ofisi nyeti ya rais. 

Donald Trump mwenye miaka 76 alifunguliwa mashitaka wiki iliyopita na baraza kuu la mahakama ya msururu wa madai yanayohusiana na malipo ya pesa yaliyotolewa kwa nyota huyo wa filamu wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2016. Mwanachama huyo bilionea aliyeanza kupiga kampeni za kuwania kurejea kwenye Ikulu ya White House katika uchaguzi ujao wa 2024, ni rais wa kwanza kuwahi kufunguliwa mashitaka ya uhalifu katika historia ya taifa hilo.

Wasaidizi wa Trump watamsindikiza akitokea kwenye makazi yake yaliyoko Mar-a-Lago, huko Florida hadi New York ambako ndiko kulikokuwa ngome ya biashara zake hapo kabla.

Akiwa huko, Trump atapitia mchakato wa kawaida, ikiwa ni pamoja na kuchukuliwa alama za vidole na kupigwa picha kama ilivyo kwa washitakiwa wengine.

Soma Zaidi: Trump kushtakiwa kufuatia malipo kwa Stormy Daniels


Trump anayetarajiwa kutoa hotuba ya hadhara kesho Jumanne kutokea Florida hata hivyo anasema madai hayo si lolote si chochote, bali ni njama tu zilizochochewa kisiasa na zinazolenga kumchafulia jina, huku akimshambulia hasa hakimu aliyepewa jukumu la kuisikiliza kesi yake.

USA, New York | Nachdem eine Grand Jury für die Anklage von Donald Trump gestimmt hat
Hali ni ya mashaka katika jiji la New York, wakati kukiwa na wasiwasi wa maandamano kati ya wafuasi na wapinzani wa Donald Trump.Picha: Selcuk Acar/AA/picture alliance

Hali ya usalama yaimarishwa New York.

Wengi wanasubiri kuona kile kitakachotokea baada ya mwanachama huyo wa chama cha Republican asiyetabirika kufika New York kwa ajili ya mchakato huo wa kisheria. Polisi ya New York iko katika hali ya tahadhari kabla ya kusikilizwa kwa mashitaka hayo yasiyo ya kawaida, lakini pia kufuatia uwezekano wa maandamano ya wafuasi na wapinzani wa Trump.

Maafisa 36,000 wameamriwa wawe tayari kupelekwa kupiga doria hii ikiwa ni kulingana na kituo cha utangazaji cha NBC, kilichonukuu vyanzo rasmi. Wakili wake Joe Tacopina alipozungumza na kituo cha televisheni cha CNN amesema wanaamini mteja wao atachukuliwa tofauti na wahalifu wengine hasa kwa kuzingatia nafasi yake na ambaye bado analindwa na idara ya usalama wa taifa, ingawa anasema Trump amejiandaa kupambana.

USA Texas | Trump Kundgebung in Waco
Wafuasi wa Donald Trump wanasema wataendelea kuwa nyuma ya kiongozi huyo bila kujali mazingira yoyote.Picha: Go Nakamura/REUTERS

Wafuasi wake wa kisiasa waapa kuendelea kusimama na Trump.

Lakini pamoja na haya yote, mRepublican huyo bado angali na wafuasi kedekede ambao wako tayari kwenda naye katika safari hii ya kuwania tena kuwa rais wa Marekani. Wengi wanasubiri kwa hamu kile atakchokizungumza kesho Jumanne huko Florida kama ambavyo ameahidi. Mmoja ya wafuasi hao kindakindaki Greg Reed akasema "Nitakwenda kokote katika pwani hii ya mashariki kumuona. Anajitoa sana kwa ajili yetu wote, nami nitajitolea kila kitu kwa ajili yake. Sikati tamaa, tunamtaka arudi tena."

Ingawa madai hasa dhidi yake bado hayajawekwa wazi, kesi hiyo iliyowasilishwa kwa jaji Alvin Bragg wa mahakama ya Manhattan yanahusisha malipo ya dola 130,000 kwa mcheza filamu huyo wa ngono Stormy Daniels kabla ya uchaguzi wa mwaka 2016.

Wakili wa zamani wa Trump na msaidizi wake Michael Cohen, alipotoa ushahidi mbele ya Baraza la Congress alimgeuka Trump na kukiri kuwa alipanga malipo kwa Daniels ili afiche ukweli kuhusu mahusiano ya kimapenzi kati yao.

Trump ambaye tayari alikuwa amemuoa Melania wakati huo, anayakana madai ya mahusiano hayo ambayo ni miongoni mwa msururu wa madai yanayochunguzwa na kuibua kitisho dhidi ya Trump na hasa katika harakati zake za kisiasa.

Sikiliza Zaidi: 

Wademocrat wazungumzia kushitakiwa rais wa zamani Trump