1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump awasili New York, kujisalimisha baadae Jumanne

4 Aprili 2023

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amewasili New York ili kujisalimisha kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka ya jinai yanayotishia kukitikisa pakubwa kinyang'anyiro cha urais wa Marekani katika uchaguzi wa mwaka 2024.

https://p.dw.com/p/4PfGA
Trump Indictment
Picha: Yuki Iwamur/AP/picture alliance

Siku ndefu ya Trump ilianza na msafara wa magari kutoka makaazi yake ya mar-a-Lago huko Florida ambapo aliabiri ndege yake ya kibinafsi iliyochorwa jina lake kwa maandishi ya rangi ya dhahabu.

Wakati wote huo wafuasi wake walikuwa wakimshangilia wakilaani mashtaka dhidi yake. Kundi dogo la wafuasi wake wengine walifanya maandamano huku wakiwa wamebeba bango lililokuwa na maandishi "Maliza Ukuta Trump24" maandishi hayo yakimaanisha Trump akamilishe azma yake ya kutaka kujenga ukuta kati ya Marekani na Mexico ili kuzuia wahamiaji atakapoingia madarakani mwaka 2024.

USA Palm Beach International Airport | Ex-Präsident Trump verlässt Florida
Ndege ya Trump ikipaa kutoka uwanja wa ndege wa Palm Beach huko FloridaPicha: Rebecca Blackwell/AP/picture alliance

Huku mji wa New York ukichukua tahadhari za kiusalama na meya wa mji huo akiwaonya wanaonuia kuleta vurugu, Trump anatarajiwa kujisalimisha mbele ya afisi ya mwendesha mashtaka wa Manhattan baadae leo na alama zake za vidole zitachukuliwa kabla kufika mbele ya jaji kusomewa mashtaka ambayo atayakanusha.

Kesi kutopeperushwa na vyombo vya habari?

Waendesha mashtaka wanasema kesi dhidi yake haina uhusiano wowote na siasa na wameitetea kazi ya mwendesha mashtaka wa Manhattan Alvin Bragg anayeiongoza kesi hiyo.

Huku akikiongezea nguvu kikosi chake cha mawakili, duru zinaarifu Trump amemuongeza Todd Blanche katika orodha ya mawakili watakaomuwakilisha katika kesi hiyo. Blanche ni wakili maarufu wa kesi za jinai na mwendesha mashtaka wa zamani wa shirikisho. 

Blanche na mawakili wengine wa Trump wamemtaka jaji katika kesi hiyo asitoe idhini ya upigaji picha, video na hata upeperushwaji katika redio kufikishwa kizimbani kwa Trump.

Katika barua kwa mahakama, mawakili hao wamehoji kuwa kukubalia tukio hilo lipeperushwe katika vyombo vya habari, kutachochea ongezeko la mazingira mabaya ya uendeshaji wa kesi hiyo na kuondolea heshima kikao hicho na mahakama.

Mahusiano na mcheza filamu za ngono

Kikosi cha walioteuliwa kumchunguza Trump, kwa miezi mwaka huu kilisikiliza ushahidi uliotolewa kuhusu dola 130,000 ambazo Trump anadaiwa kumlipa mwanamke mmoja mcheza filamu za ngono Stormy Daniels katika siku za mwisho za kampeni ya mwaka 2016. Trump aliushinda uchaguzi huo na kuwa rais wa Marekani.

USA Florida | Exxxotica Miami 2012 | Stormy Daniels
Nyota wa filamu za ngono Stormy DanielsPicha: SMG/ZUMA Wire/picture alliance

Daniels anasema alilipwa ili asifichue taarifa kuhusu mahusiano ya kingono aliyokuwa nayo na Trump katika hoteli moja mwaka 2006. Trump lakini anakunasha kuwa na mahusiano yoyote na mwanamke huyo.

Baada ya kusimama kizimbani, afisi ya Trump imesema atarudi nyumbani kwake Florida ambapo katika mkutano na waandishi wa habari, atatoa maoni kuhusiana na yaliyojiri.

Rais huyo wa zamani wa Marekani anasema kwamba kesi hiyo ni hujuma za kisiasa za Wademocrat kuelekea uchaguzi wa mwaka 2024. Trump tayari ashatangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Republican.

Chanzo: /Reuters/AP/AFP