1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump, Biden wajadili vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati

14 Novemba 2024

Rais mteule wa Marekani Donald Trump aliwasili katika Ikulu ya White House kwa mara ya kwanza tangu aliposhinda uchaguzi wa wiki iliyopita na kukaribishwa na rais wa sasa Joe Biden.

https://p.dw.com/p/4mypG
USA | Joe Biden trifft Donald Trump
Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Mbali na kuzungumzia makabidhiano ya amani ya madaraka, Trump na Biden ambao ni mahasimu wa muda mrefu wa kisiasa, walijadili pia mizozo inayoendelea duniani ikiwa ni pamoja na vita vya Ukraine na Mashariki ya Kati.

Marais hao wawili ambao ukijumuisha umri wao unafikia miaka 159 walisalimiana huku Biden akionekana kutazama chini, wakati Trump akisimama kwa kujiamini na kumtazama Biden machoni.

Biden amkaribisha Trump Ikulu ya White House

Hata hivyo rais Biden amempongeza Trump kwa ushindi wake, wakati alimpokaribisha katika ofisi ya rais na kusalimiana naye kwa kushikana mikono, akimuahidi mchakato mzuri wa kumkabidhi mamlaka. Ikumbukwe kuwa miaka minne iliyopita, baada ya kushindwa katika uchaguzi, Trump alikataa kushiriki katika utaratibu huo wa kukabidhiana madaraka.

Msemaji wa Ikulu ya White House Karine Jean-Pierre, aliwaeleza waandishi wa habari kwamba viongozi hao wawili wamejadili masuala muhimu kuhusu usalama wa kitaifa na sera za ndani zinazolikabili taifa la Marekani na ulimwengu kwa ujumla. 

Sullivan asema Biden alimsisitizia Trump kwamba ni muhimu kuendeleza uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine 

USA | Jake Sullivan | mshauri wa usalama wa kitaifa
Mshauri wa usalama wa kitaifa nchini Marekani Jake SullivanPicha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Naye mshauri wa usalama wa kitaifa Jake Sullivan amesema Biden alimsisitizia Trump kwamba ni muhimu kuendeleza uungaji mkono wa Marekani kwa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi. 

Kulingana na Sullivan, Biden amesema uungaji mkono kwa Ukraine ni bora kwa usalama wa taifa wa Marekani kwa sababu uwepo wa bara la Ulaya lililo imara na thabiti kutazuia nchi hiyo kujiingiza katika vita.

US kuiongezea Ukraine misaada kabla ya Trump kuingia madarakani

Itakumbukwa kuwa Trump ambaye anaendelea kupanga safu yake ya uongozi, aliahidi kuvimaliza kwa haraka vita vya Urusi na Ukraine bila hata hivyo kueleza ni jinsi gani angelifanikisha hilo. Rais huyo mteule amelieleza pia gazeti la New York Post kwamba yeye na Biden walizungumzia sana kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati kwani alitaka kufahamu ni wapi walipofikia.

Viongozi hao wawili wamekutana wakati matokeo ya uchaguzi yakiwa yamekiwezesha chama cha Republican kudhibiti mabunge yote mawili ya Baraza la Wawakilishi na Seneti na hivyo kuashiria kuwa Trump hatokuwa na vikwazo kutekeleza sera na mipango yake.
 

Trump: Ushindi huu ni mageuzi makubwa ya kisiasa