Tshisekedi akataa mazungumzo ya moja kwa moja na M23
19 Januari 2025Kauli hii inajiri baada ya mkutano uliotarajiwa kufanyika tarehe 15 Disemba nchini Angola kati ya Tshisekedi na Rais wa Rwanda Paul Kagame kufutwa wakati pande hizo mbili hazikuweza kukubaliana kuhusu masharti ya mazungumzo hayo.
Tshisekedi aliwaambia wanadiplomasia mjini Kinshasa kwamba mazungumzo hayo yameshindwa kwa sababu ya ujumbe wa Rwanda kutowa sharti jipa la kutaka yafanyike mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi la waasi la M23.
Soma pia: UN: Zaidi ya watu 230,000 wamekimbia ghasia mashariki mwa DRC tangu Januari 1
Siku ya Alhamisi, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Angola Joao Lourenco walitoa wito wa kuanzishwa tena kwa mazungumzo katika ngazi ya juu kati ya DRC na Rwanda. Lakini Tshisekedi alisema nchi yake haitakubali kile alichokitaja kama "shinikizo kutoka nje" kuweka masharti ambayo yanakiuka kanuni na mamlaka ya Kongo.