UN: Watu 230,000 wamekimbia ghasia mashariki mwa DRC
18 Januari 2025Eujin Byun, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva hapo jana kuwa, kuongezeka kwa mapigano kati ya jeshi la Kongo na makundi yenye silaha katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, kunachochea moja ya majanga ya kibinadamu ya kutisha zaidi duniani lakini ambayo hayaangaziwi ipasavyo.
Msemaji huyo wa UNHCR ameongeza kuwa mgogoro huo unajumuisha vitendo mbalimbali vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na kuwalazimisha watu wengi kuyahama makazi yao. Byun alidokeza kuwa majimbo mawili ya Kivu kaskazini na Kusini tayari yana watu milioni 4.6 waliokimbia makazi yao, na hivyo kuifanya DRC kuwa mojawapo ya nchi duniani yenye wakimbizi wa ndani.
Soma pia: UN: Karibu watu milioni moja wameyahama makazi yao DRC
Wakaazi wa vijiji viwili katika mkoa huo, Kabingo na Ruzirantaka, wameliambia shirika la habari la AFP kwa njia ya simu kwamba, siku ya Ijumaa kulikuwa na mapigano na milipuko ya mabomu.
Byun amesema mapigano makali katika maeneo ya Masisi na Lubero yamewalazimu takriban watu 150,000 kuyakimbia makazi yao kati ya Januari 1 na 6 mwaka huu. Maelfu wengine walikuwa wamerejea nyumbani wakati kuliposhuhudiwa utulivu wa muda mnamo Januari 4, lakini walilazimika kukimbia tena siku chache baadaye wakati mapigano mapya yalipozuka.
UNHCR: Raia wanakabiliwa na hali mbaya
Kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda, ambalo sasa linachukuliwa kama kundi la kigaidi na serikali mjini Kinshasa, limechukua udhibiti wa maeneo mengi mashariki mwa DRC, eneo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali na lililokumbwa na migogoro kwa miaka 30.
Katika wiki za hivi karibuni, kundi hilo la waasi wa M23 limepata nguvu zaidi na mapema mwezi huu lilidhibiti mji mkuu wa eneo la Masisi katika jimbo la Kivu Kaskazini. Jeshi la Kongo limeapa kuchukua tena udhibiti wa maeneo yote na limekuwa likifanya mashambulizi ya kukabiliana na kundi hilo.
Soma pia: MSF: Wakimbizi wa ndani Kongo wakabiliwa na ukatili
Katika eneo la Fizi huko Kivu Kusini, mamlaka za eneo hilo zimeomba msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na kueleza kwamba watu 84,000 walikuwa wamekimbilia huko. Byun ameonya kwamba raia wakikabiliwa na miripuko ya mabomu na unyanyasaji wa kijinsia na kwamba watoto pia wamekuwa wakilengwa na vitendo hivyo.
"Hali ya kibinaadamu ambayo tayari ni mbaya inazidi kuwa mbaya zaidi na kwa kasi, na ufikiaji wa watu hao walio katika mazingira magumu unatatizwa na ukosefu wa usalama, vizuizi vya barabarani na uwepo wa makundi yenye silaha," alisema Byun.
UNHCR imesema iko tayari kutoa msaada kwa watu hao mara tu ufikiaji wao utakapowezeshwa, lakini imesisitiza kuwa fedha zaidi zinahitajika. Shirika hilo limesema linahitaji dola milioni 226 kutoa msaada nchini DRC mwaka huu, lakini hadi sasa, chini ya asilimia 10 ya kiasi hicho ndio iliyopatikana.
(Chanzo: AFP)