1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tume ya IEBC yaandamwa kuhusu karatasi za kupigia kura

8 Julai 2022

Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC inaandamwa na shinikizo za kisheria baada ya kuanza kuchapisha makaratasi ya kupigia kura Kabla ya wagombea wa urais kuorodheshwa kwenye gazeti rasmi la serikali.

https://p.dw.com/p/4DqeL
Kenia | Präsidentschaftswahlen
Picha: Shisia Wasilwa/DW

Saa chache baada ya shehena ya kwanza ya makaratasi ya kupigia kura kuwasili nchini Kenya, tume ya uchaguzi na mipaka IEBC sasa imejikuta pabaya kisheria. Kulingana na mchakato wa uchaguzi, majina ya wagombea wa urais yanapaswa kuorodheshwa kwenye gazeti rasmi la serikali Kabla ya makaratasi ya kupigia kura kuanza kuchapishwa. Mawakala wa wagombea wa urais wameelezea wasiwasi wao na kuwa huenda hilo likaufungua mwanya wa kesi Mahakamani.

Karatasi za Kura zaanza kuwasili nchini Kenya

Kwa upande wake tume ya uchaguzi inajitetea kuwa mchapishaji wa serikali ndiye aliyeichelewesha ratba hiyo na kwamba orodha rasmi iliyotiwa saini iliwasilishwa kwao mwishoni mwa Juni. Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukatiamefafanua hayo.

Wakati huohuo IEBC inatuhumiwa kwa kuwa na usiri Mwingi mintarafu maelezo Kamili ya mchakato wa uchaguzi kama vile orodha Kamili ya daftari la wapiga kura na pia mfumo wa kuhesabu kura na kutangaza matokeo.

Duru zinaeleza kuwa tume ya uchaguzi inajiandaa kutumia picha za fomu za matokeo ya uchaguzi badala ya takwimu za hesabu ya kura kama msingi wa kukusanya matokeo ya uchaguzi. Hilo limezusha mitazamo tofauti kwani huenda shughuli ya kutangaza matokeo ikajikokota. Ili kuituliza hali, IEBC imeweka bayana kuwa mawakala wa wagombea wa urais watasafiri hadi Ugiriki kati ya tarehe 15 na 20 mwezi huu wa Julai kushuhudia makaratasi ya kupigia kura yakichapishwa.

Kwa upande mwengine, Azimio la Umoja One Kenya inasisitiza kuwa hawatasusia uchaguzi hata baada ya kuelezea wasiwasi wao kuhusu matumizi ya daftari asilia la wapiga kura. Muungano wa Kenya Kwanza unanadi sera zake eneo la kaskazini.