1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Uamuzi wa mahakama ya UN kuhusu Kabuga wakosolewa

9 Agosti 2023

Walionusurika na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 wamekosoa uamuzi uliotolewa na Makahama ya Rufaa ya Umoja wa Mataifa kutaka mtuhumiwa wa mauaji hayo Felicien Kabuga, kuachiliwa huru kwa sababu za kiafya.

https://p.dw.com/p/4UwjE
Felicien Kabuga
Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994, Felicien KabugaPicha: Handout/MICT/AFP

Kundi linalowawakilisha watu walionusurika na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 wameelezea kugadhabishwa na kusikitishwa na uamuzi uliotolewa na majaji wa Makahama ya Rufaa ya Umoja wa Mataifa kutaka mtuhumiwa wa mauaji hayo Felicien Kabuga, kuachiliwa huru kwa sababu hana uwezo wa kiafya na kimwili kusimama kizimbani kujibu mashtaka yanayomkabili.

Uamuzi umeamsha majeraha makubwa

Kundi hilo linalojulikana kama Ibuka, limeukosoa uamuzi huo likisema kuwa ni tusi la makusudi na kwa majeraha makubwa ambayo wanayapitia walionusurika na mauaji hayo. Naphtali Ahishakiye, katibu mtendaji wa kundi la Ibuka, ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba walionusurika wamekatishwa tamaa na uamuzi kuhusu uwezekano wa kuachiwa huru Kabuga, na hilo ni jambo la kusitikisha.

Niederlande I Völkermord Prozess vor Gericht in Den Haag
Mafuvu ya baadhi ya waliouawa wakiwa wamejihifadhi kwenye kanisa moja Ntarama, RwandaPicha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Mwezi Juni, majaji wa Mahakama ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kesi ya Uhalifu, IRMCT walisema hakuna uwezekano wa Kabuga kutiwa hatiani kwa sababu hana uwezo wa kiafya na kiakili kusimama kizimbani, na badala ya kuiondoa kesi yake mahakamani, wataandaa utaratibu mwingine wa kisheria kwani hawezi kushiriki tena kesi yake kikamilifu.

Kabuga, aliyekuwa mfanyabiashara tajiri, anatuhumiwa kwa kuanzisha redio na televisheni iliyokuwa ikichochea chuki na kuwataka Wahutu kuwaua Watusti kwa mapanga na kusababisha kutokea kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambapo takribani watu 800,000 waliuawa.

Majaji wataka uamuzi uzingatiwe

Siku ya Jumatatu, majaji wa Mahakama ya Rufaa walisema kuwa mahakama ya mwanzo ilifanya ''kosa la kisheria'' na uamuzi wa Kabuga, mwenye umri wa miaka 88 kwa mujibu wa maafisa, ingawa mwenyewe anadai ana miaka 90, unapaswa kuzingatiwa kwa haraka ili aweze kauchiliwa huru.

Mwendesha Mashtaka mkuu wa mahakama hiyo, Serge Brammertz, amesema alipitia kwa uangalifu uamuzi wa Mahakama ya Rufaa na kusisitiza kuwa uamuzi huo lazima uheshimiwe, hata ingawa matokeo yake hayaridhishi. ''Nawafikiria walionusurika na mauaji hayo, najua wazi kuwa uamuzi huo unafadhaisha na kukatisha tamaa,'' alifafanua Brammertz. Wakili wa Kabuga, Emmanuel Altit, amesema amefurahishwa na uamuzi huo wa majaji wa rufaa.

Niederlande | Prozess in Den Haag Ruanda Genozid Felicien Kabuga
Wakili wa Felicien Kabuga, Emmanuel Altit (katikati)Picha: Koen van Weel/REUTERS

Ahishakiye amesema kundi la Ibuka sasa linafikiria kusitisha uhusiano wake na mahakama ya IRMCT. Amesema kuendelea kushirikiana na mahakama inayowalinda wahalifu wa mauaji ya kimbari kwa gharama ya haki ya walionusurika, hakuna maana.

Walionusurika wanahisi ulimwengu umewatupa

Mmoja wa watu walionusurika na mauaji ya kimbari ya Rwanda, Francine Uwamariya amesema anahisi ulimwengu hauwatakii mema. ''Kilicho muhimu kwao ni angalau kupata haki,'' alisisitiza Francine ambaye amesema amepoteza familia yake yote mikononi mwa wafuasi wa Kabuga.

Kabuga alikamatwa mjini Paris, mwaka 2020 baada ya kutafutwa kwa zaidi ya miongo miwili na kupandishwa kizimbani mwezi Septemba, mwaka uliopita. Hata hivyo, amekana kuhusika na mauaji hayo na majaji walisema mwezi Juni kwamba wataalamu wa afya waligundua Kabuga alikuwa na matatizo makubwa ya kusahau.

(AFP, AP, DPA)