1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ubora soka la Ujerumani wafika ukingoni?

2 Desemba 2022

Vyombo vya habari vya Ujerumani vinahoji kama Ujerumani itabakia kuwa taifa kubwa katika ulimwengu wa soka. Baada ya kuondolewa katika hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Dunia, mengi yanaandikwa.

https://p.dw.com/p/4KP4j
FIFA Fußball WM 2022 in Katar | Spanien - Deutschland
Picha: Christian Charisius/dpa/picture alliance

Kwa mara ya pili mfululizo timu ya taifa ya Ujerumani imeondolewa katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Dunia. Vyombo vya habari vya Ujerumani vimejikuta katika sintofahamu  na kinachoshuhudiwa sasa ni lawama zinazotoka kila upande. 

Mengi yamehanikiza hii leo katika magazeti ya Ujerumani baada ya timu ya taifa kung'olewa. Vichwa vya habari kwa mfano kwenye gazeti la Spiegel kilisomeka "Ilikuwa ni kama milimita, lakini ulikuwa umbali mrefu". Na kichwa kingine cha habari kiliandika "walikaribia, lakini bado walikuwa mbali sana"

Vichwa hivi vya habari vilikuwa vikimaanisha namna goli la Japan dhidi ya Uhispania lilivyowazamisha miamba hao wa soka na kuhitimisha mbio za Ujerumani katika hatua ya mwanzo kabisa ya makundi, tena kwa mara ya pili mfululizo.

Kituo cha habari cha Ujerumani cha ARD kilimuuliza mchezaji wa Die Mannschaft Kai Havertz aliyetokea benchi na kuifungia mabao mawili kati ya manne dhidi ya Costa Rica, kwamba ni kwa kiasi gani aliichukia Uhispania? Walimuuliza hivi, kwa sababu kinyume na matarajio, Japan iliifunga Uhispania mabao 2-1. Vinginevyo, ushindi wa Uhispania, ungewapa fursa ya kusonga mbele.

WM 2022 - Costa Rica - Deutschland
Kai Havertz akiifungia bao la kwanza Die Mannschaft ilipopambana na Costa Rica.Picha: Matthew Childs/REUTERS

Lakini hata hivyo, wachezaji wenyewe wanatambua fika kwamba sio Uhispania inayotakiwa kulaumiwa hapa, bali ni wao wenyewe waliosabababisha kishindo hiki ambacho gazeti la Bild la Ujerumani limeandika "mwisho wa lililowahi kuwa taifa kubwa kisoka; mabingwa mara nne wa Kombe la Dunia na mara tatu, Barani Ulaya.

Gazeti ndugu la Bild la michezo nalo liliibuka na habari iliyoonyesha kutoamini kilichotokea. Liliandika "Baada ya Urusi mwaka 2018, tulidhani hali haitakuwa mbaya zaidi. Lakini sasa tunajua itakuwa. Ni janga. Ujerumani imeporomoka"

Na meza ya michezo ya hapa DW, mwandishi wake Jonathan Harding aliyekuwa huko Qatar aliandika " Ujerumani haitambuliki tena kama timu ya viwango vya juu"

Sasa mwelekeo ni upi kutokea hapa? Jarida maarufu la Kicker la masuala ya soka la hapa Ujerumani limeandika "ni mashaka katika ngazi zote". Likaandika, lawama zinakwenda kwa kila mmoja, kuanzia kocha mkuu Hansi Flick mkurugenzi wa michezo Oliver Bierhoff hadi rais wa Shirikisho la Soka la Ujerumani, DFB, Bernd Neuendorf.

Gazeti jingine la Süddeutsche Zeitung likaliunga mkono Kicker likiyalezea matokeo haya kuwa yanakwenda sambamba kabisa na mkanganyiko wa mambo uliopo.

Likasema kocha Flick anapaswa kulaumiwa moja kwa moja kwa kufanya mabadiliko ya mara kwa mara kwenye eneo la  ulinzi, lakini pia kuchelewa kumuingiza Niclas Füllkrug.

Fußball | WM Qualifikation | Deutschland - Liechtenstein | Joachim Löw
Kocha wa Ujerumani aliachia ngazi baada ya kikosi chake kuondoshwa kwenye michuano ya Euro ya mwaka 2020.Picha: Markus Gilliar/GES/picture alliance

Oliver Bierhoff, mkurugenzi wa michezo wa DFB naye ananyooshewa kidole. Mkurugenzi huyu kwa miaka 18 sasa na ambaye imani yake kwa kocha mtangulizi wa Flick, Joachim Loew aliyeondoka kwa aibu katika michuano ya mwaka 2018 huko Urusi, iliendelea kusababisha majanga si tu kwenye michuano ya Euro ya mwaka 2020 dhidi ya England bali hata sasa katika michuano inayoendelea huko Qatar.

Lakini waandishi wengine wanapeleka lawama zao nje ya uwanja. Kwa mfano mtangazaji wa ARD Esther Sedlaczek alizungumza na Bierhoff kuhusiana na suala tata la nahodha wa Die Mannschaft kuvaa mkononi kitambaa chenye alama za mapenzi ya jinsia moja, na namna lilivyowavuruga wachezaji, kwa kuwa sio wote waliokuwa wakiunga mkono suala hilo na hivyo kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Japan huku kukiwa na mgawanyiko.

Lakini mkurugenzi huyo wa michezo alimshangaa mtangazaji huyo kwa kuamini suala hilo limechangia kushindwa kwao, hata baada ya michezo yao mitatu, na kuhitimisha kwamba hilo halikuchangia chochote.

Lakini gazeti la Bild likahitimisha kwamba, kama wachezaji wangekuwa na ujasiri wa kuvaa vitambaa hivyo, basi mamilioni ya mashabiki wa Ujerumani angalau wangekuwa na kitu cha kujivunia kuhusu timu yao ya taifa.

DW