Uchumi wa Ujerumani huenda ukaimarika kwa kujikongoja
15 Mei 2024Tathmini kutoka kwa baraza la serikali la washauri wa kiuchumi inaendana na utabiri mwingine wa hivi karibuni ambao ulisema kuwa uchumi wa taifa hilo lenye nguvu kiuchumi katika kanda ya Ulaya unaanza kuimarika taratibu.
Pato la mwaka jana lilipungua kidogo kutokana na kuongezeka kwa mfumuko wa bei, kushuka kwa sekta muhimu ya utengenezaji bidhaa na mahitaji duni kutoka kwa washirika wakuu wa biashara, na haswa China.
Soma: Nusu ya makampuni ya Ujerumani yakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi
Licha ya changamoto zinazoendelea, wataalam wanatarajia "uchumi wa Ujerumani kushika kasi katika kipindi cha 2024," amesema mmoja wa wajumbe wa baraza hilo Martin Werding.
Kuongezeka kwa usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi kulikochochewa na kurejesha biashara ya kimataifa, pamoja na kuboresha mahitaji ya watumiaji kutokana na kuongezeka kwa mishahara ambako kumeleta ahueni, imesema ripoti hiyo.
Hata hivyo wataalam wanatarajia ongezeko tu la wastani, kwa asilimia 0.2 katika pato la taifa (GDP) mwaka huu kabla ya ongezeko la asilimia 0.9 mwaka 2025.
Serikali ilitabiri ukuaji wa asilimia 0.3 mnamo 2024.
Viashiria vya uchumi, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa viwandani, tafiti za biashara, vimekuwa vikiongezeka katika miezi ya hivi karibuni.
Uchumi: Kuzorota uchumi wa Ujerumani ni changamoto kwa Ulaya ya kati
Lakini ukuaji wa uchumi wa Ujerumani bado utakuwa chini ukilinganishwa na eneo pana la mataifa 20 linalotumia sarafu ya Euro, ambalo Umoja wa Ulaya, unatabiri kuwa utakuwa kwa asilimia 0.8 mwaka 2024.Dalili zaonesha uchumi wa Ujerumani utaboreka 2024
"Kampuni za Ujerumani zinazoelekeza mauzo ya nje zinakabiliwa na ushindani mkali, kupanda kwa gharama za kuwahudumia wafanyakazi na kuendelea kupanda kwa bei ya nishati," alisema mjumbe mwingine wa baraza Veronika Grimm.