1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa, Ujerumani, Uingereza zataka Urusi iwekewe vikwazo

Yusra Buwayhid
8 Oktoba 2020

Ujerumani na Ufaransa zimeinyooshea kidole cha lawama serikali ya Urusi na kuishutumu kwa kuhusika katika kumuwekewa sumu mkosoaji wa serikali, Alexei Navalny

https://p.dw.com/p/3jdoZ
Russland Sankt Petersburg | Demo Solidarität mit Nawalny
Picha: picture-alliance/dpa/Tass/P. Kovalev

Mataifa ya Ulaya yameitaka mara kadhaa Urusi kutoa maelezo zaidi juu ya mkasa huo wa kuwekewa sumu Navalny uliofanyika kwenye ardhi ya Urusi, lakini kulingana na taarifa ya pamoja iliyotolewa na mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na Ufaransa, "hakuna maelezo ya kuaminika ambayo yametolewa na Urusi hadi sasa." Soma pia: Navalny aapa kurudi Urusi

Haraka Urusi iliwajibu kwa kuyakana madai hayo na kusema kwamba hayakubaliki. Msemaji wa Rais Vladimir Putin, Dmitry Peskov, alisema hapo jana kwamba wataalamu wa Shirika la Kudhibiti Silaha za Kemikali (OPCW) watapatiwa kila wanachokihitaji katika uchunguzi wao wa madai ya kupewa sumu Alexei Navalny.

Lakini pia Peskov aliongeza Urusi haiwezi kuwa imehusika na tukio hilo, kwani ni mwanachama wa shirika la OPCW ambalo linakataza matumizi ya kemikali zilizotumiwa dhidi ya Navalny:

Alexej Nawalny mit Frau und Sohn in Berlin
Navalny na mkewe na mwanawe wa kiumePicha: Instagram @Navalny/Reuters

"Kwa hakika serikali Urusi ingependa kutoa ufafanuzi juu ya kilichotokea Omsk. Lakini sumu hiyo haitogunduliwa kwetu kutokana na kwamba serikali ya Urusi ni mwanachama wa mikataba inayokataza silaha za kemikali.Shirikisho la Urusi limetekeleza wajibu wake chini ya mikataba hii. Kwahivyo hilo haliwezekani" Soma pia: Jengo, akaunti za Navalny vyazuiwa

Naye waziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Dominic Raab, ameishutumu Urusi kwa kuhusika na tukio hilo, na kusema kwamba Uingereza itafanya kazi pamoja na washirika wake wa kimataifa, ili kuwawekea vikwazo maafisa wa urusi na wengineo waliohusika.

Kauli kali kutoka mataifa ya Ulaya zimeanza kutolewa baada ya shirika hilo la kudhibiti silaha za kemikali la Umoja wa Mataifa OPCW kuthibitisha kilichogunduliwa na Ujerumani, Ufaransa na Sweden, kwamba Navalny alipewa sumu ya aina ya Novichok iliyotengenezwa Urusi.

Daima Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuwa na mazungumzo yenye uwazi pamoja na Putin, lakini amebadilisha msimamo wake huo katika miezi ya hivi karibuni.

Navalny mwenye umri wa miaka 44 na ambaye anaendelea kupatiwa matibabu mjini Berlin, Ujerumani, ameusisitiza Umoja wa Ulaya kuchukua hatua ikiwa ni pamoja kuwapiga marufuku maafisa muhimu wa Urusi pamoja na wale wanaoiunga mkono serikali ya Putin kuingia katika nchi za Ulaya. 

afp,ap, dpa, reuters