1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda kusaidia ujenzi wa barabara Congo

29 Septemba 2020

Serikali ya Uganda imesema Jumanne kuwa itasaidia kufadhili miradi ya ujenzi wa zaidi ya kilomita 200 za barabara ndani ya DRC kama sehemu ya mipango ya kuboresha biashara kati ya mataifa hayo.

https://p.dw.com/p/3jBGY
Uganda EU AMISOM Friedenstruppe General Katumba Wamala
Picha: DW/E. Lubega

Uganda itachangia karibu asilimia 20 ya thamani ya mradi huku kiasi kingine kikitolewa na serikali ya Congo katika mradi wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi, waziri wa ujenzi na usafiri wa Uganda Jenerali Katumba Wamala (pichani juu) aliliambia shirika la habari la Associated Press.

Soma pia:Rwanda na Uganda Matatani

Utaratibu kama huo siyo wa kawaida katika eneo ambako serikali zinapambana kupanua mitandao ya barabara ndani ya mipaka yake. Licha ya ukubwa wake na utajiri wa rasilimali, Congo inasalia kuwa moja ya mataifa maskini zaidi duniani. Eneo la mashariki mwa nchi hiyo limegubikwa hasa na vurugu za makundi ya waasi.

Soma pia: Mkutano wa Kampala na majaaliwa ya Kongo

"Wakati wote kuna mara ya kwanza kwa kila kitu," Wamala alisema. "Huu ni mradi wa pamoja kati ya nchi mbili na kuna sababu nzuri tu ya hilo."

Ofisi ya msemaji wa serikali ya Uganda ilisema katika taarifa kwamba mkutano wa baraza la mawaziri uliidhinisha utengenezaji au ukarabati wa barabara kutoka mpakani hadi mji wa Congo wa Beni, pamoja na barabara kutoka kituo cha mpakani cha Bunagana hadi mji wa Goma.

Afrika Uganda l Katuna - Grenze zu Ruanda
Uganda imeelezea kufungwa kwa mpaka kati yake na Rwanda kama vikwazo vya biashara.Picha: DW/A. Gitta

Miradi hiyo itaimarisha uwekezaji na kuboresha usalama mashariki mwa Congo, ilisema taarifa hiyo.

Mzozo kati ya Uganda na Rwanda

Uamuzi wa Uganda kushirikiana na Congo unakuja wakati wa mkwamo na nchi jirani ya Rwanda, ambayo kwa wakati mmoja ilikuwa kituo kikuu cha mauzo ya nje ya nafaka na mazao mengine kutoka Uganda.

Soma pia: Museveni kuwachukulia hatua wanajeshi wa Rwanda

Serikali ya Rwanda ilifunga mpaka wake na Uganda wenye shughuli nyingi mnamo mwezi Februari 2019, katika kile ambacho Uganda inakielezea kama vikwazo vya kibiashara. Serikali ya Rwanda iliwaamuru raia wake kutosafiri kwenda Uganda, ikidai kwamba raia wa Rwanda hawakuwa salaama ndani ya mipaka ya nchi hiyo.

Soma pia: Uganda yakanusha kusaidia kundi la upinzani Rwanda

Maafisa wa Rwanda pia waliituhumu serikali ya Uganda kwa kuunga mkono waasi wanaompinga rais Paul Kagame. Maafisa wa Uganda nao wakawatuhumu mawakala wa serikali ya Kigali kwa kuendesha operesheni zao kinyume na sheria nchini Uganda, ikiwemo katika madai ya utekaji nyara wa raia wanaotafutwa nchini Rwanda.

Chanzo: APE