1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

Uganda yawatia hatiani kwa "uhaini" wanachama 16 wa upinzani

22 Oktoba 2024

Mahakama ya kijeshi nchini Uganda imewatia hatiani siku ya Jumatatu wanachama 16 wa chama cha upinzani kwa kosa la "uhaini" na umiliki wa vilipuzi kinyume cha sheria.

https://p.dw.com/p/4m4hl
Polisi wa Uganda wakiwa nje ya jengo la chama cha NUP mjini Kampala
Polisi wa Uganda wakiwa nje ya jengo la chama cha NUP mjini KampalaPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Taarifa hiyo ni kulingana na wakili wa upande wa utetezi Shamim Malende, ambaye amesema kesi hiyo ilikuwa na mashaka kutokana na jinsi ilivyosikilizwa na baadaye watuhumiwa kukubali makosa ambayo awali waliyakana.

Upande wa mashtaka umedai kuwa wanachama 16 wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP), pamoja na wengine ambao bado hawajakamatwa, walikutwa na vilipuzi kati ya Novemba mwaka 2020 na Mei 2021, wakati uchaguzi ulikuwa ukiendelea.

Soma pia: Uganda: Polisi yasitisha mikutano ya siasa ya Bobi Wine

Waandishi wa habari hata hivyo hawakuruhusiwa kuhudhuria kikao hicho. Vijana hao 16 wamekaa gerezani kwa miaka minne, na watafikishwa mahakamani hapo kesho ili kusomewa rasmi hukumu yao.

Kauli za kiongozi mkuu wa upinzani

Kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine
Kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi WinePicha: Hajarah Nalwadda/AP/picture alliance

Mwimbaji wa zamani na kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama  Bobi Wine , amedai kuwa watu hao walilazimishwa kukiri makosa yao na kuomba msamaha wa rais.

"Chochote ambacho serikali ya Museveni inafanya, siku moja wale wote walio chini yake akiwemo yeye mwenyewe watawajibishwa" alisema Bobi Wine kuliambia shirika la habari la AFP, akisisitiza kuwa washtakiwa "walilazimishwa na maafisa wa serikali kukubali makosa hayo".

Tangu mwaka 1986, Uganda imetawaliwa na rais  Yoweri Museveni . Uchaguzi uliopita wa urais wa mwaka 2021 ulikumbwa na kashfa ya udanganyifu, na maandamano ya kupinga kukamatwa tena kwa Bobi Wine yalikandamizwa vikali na polisi, na kusababisha takriban watu 54 kuuawa.

(Chanzo: AFP)