1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Uhaba wa mafuta watatiza shughuli za kiutu Gaza

Sylvia Mwehozi
14 Novemba 2023

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limeonya kwamba bohari yake ya mafuta imekauka na huenda wakalazimika kusimamisha shughuli zake ndani ya saa 48.

https://p.dw.com/p/4YlZ8
Flüchtlingscamp NRWA
Picha: Mustafa Hassona/AA/picture alliance

Mkuu wa shirika hilo Thomas White aliandika kupitia ukurasa wa X kwamba "operesheni za kiutu huko Gaza huenda zikasimama ndani ya kipindi hicho kwa kuwa hakuna mafuta yanayoruhusiwa kuingizwa Gaza".

Soma kwa kina taarifa ifuatayo: UN yawakumbuka watumishi wake waliouawa kwenye vita vya Mashariki ya Kati

Ameongezea kuwa UNRWA imekuwa ikitumia mafuta kutoka katika hifadhi yake lakini nako mafuta yamewaishia na hakuna mafuta yaliyoruhusiwa kuingia Gaza tangu Oktoba 7 wakati Hamas walipofanya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel.

Baadae DW ilizungumza na mkuu wa kitengo cha mawasiliano na mahusiano ya nje wa shirika hilo Tamara Alrifai, aliyesema kuwa hali katika Ukanda wa Gaza itakuwa ya "maafa" ikiwa hakuna usitishwaji wa mapigano.

Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas pia ilisema mapema Jumatatu kwamba hospitali zote kaskazini mwa Gaza hazifanyi kazi tena kutokana na uhaba wa mafuta.

Israel -Gaza -Majeruhi
Madaktari wakiwahudumia majeruhi GazaPicha: Ashraf Amra/Andalou/picture alliance

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito kwa Israel wa kuilinda hospitali kubwa ya Al-Shifa katika Ukanda wa Gaza wakati shirika la afya ulimwenguni WHO likisema hospitali hiyo haifanyi kazi tena. 

Wafanyakazi katika hospitali hiyo wamedai kuzingirwa, baada ya kituo hicho kushambuliwa mara kadhaa kwa mabomu na kuongeza kuwa Israel inawapiga risasi watu wanaotoka nje ya jengo hilo.

Hata hivyo Israel imekanusha madai hayo, ikisema Hamas inatumia mtandao wa mahandaki chini ya hospitali hiyo, ingawa haijatoa ushahidi wowote kuhusu hilo.

Soma kwa kina kuhusu mada hii:Hosptali kubwa ya Gaza yakabiliwa na mashambulizi ya karibu 

Wakati hayo yakiripotiwa, jeshi la ulinzi la Israel IDF, limesema kuwa linaendelea na msako mkali kwenye viunga vya kambi ya wakimbizi ya al-Shati ndani ya Gaza City.

IDF ilisema vikosi vyake vilikuwa "vinailenga miundombinu ya kigaidi iliyoko katika taasisi za serikali kuu katikati mwa raia, zikiwemo shule, vyuo vikuu, misikiti na makazi ya magaidi."

Mzozo wa Hamas na Israel
Wanajeshi wa Israel wakati wa operesheni yake ya ardhiniPicha: Israeli Defense Forces/REUTERS

Aidha taarifa ya jeshi hilo iliyotolewa kupitia mtandao wa Telegram imesema wanajeshi wake waliingia kwenye makazi ya mwanachama wa ngazi za juu wa kundi la Islamic Jihad na kukuta "idadi kubwa ya silaha kwenye chumba cha watoto."

Islamic Jihad ni kundi dogo la wanamgambo linalofanya oparesheni zake huko Gaza na lenye mafungamano na Hamas. Marekani, Umoja wa Ulaya na serikali nyingine zinaitaja Hamas kama shirika la kigaidi.Israel yaendeleza mashambulizi yake Gaza

Kwa mujibu wa wizara ya Afya inayoongozwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 11,000 wameuawa tangu vita kuanza.

Hapo jana, jamaa za watu waliochukuliwa mateka na kundi la Hamas wakati wa mashambulizi yake ya Oktoba 7 dhidi ya Israel, walikusanyika mjini Jerusalem kuutaka Umoja wa Mataifa kushinikiza juu ya kuachiliwa huru. Waandamanaji walibeba picha za wapendwa wao ambao mpaka sasa wanashikiliwa huko Gaza.

Kauli ya Netanyahu: Netanyahu asema kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kuachiwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas

Wakati huohuo pia, wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani imesema zaidi ya raia wake 290 wamefanikiwa kuondoka Gaza kupitia kivuko cha Rafah kuingia Misri.

Msemaji wa wizara hiyo mjini Berlin alisema kuwa takriban raia 400 wa Ujerumani bado wako katika maeneo ya Palestina, ukiwemo Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.