1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Somalia na Kenya mashakani

Thelma Mwadzaya15 Desemba 2020

Kenya na Somalia zimeingia kwenye kipindi kigumu cha uhusiano wa kidiplomasia. Ili kuipoza hali, Kenya inajiandaa kutuma kikosi cha usuluhishi baada ya Somalia kutangaza kuvunja uhusiano wake na Kenya usiku wa Jumanne.

https://p.dw.com/p/3mkfe
Kenia Nairobi Besuch Somalischer Präsident
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Kwenye Kikao na waandishi wa habari, msemaji wa serikali Cyrus Oguna aliweka bayana kuwa Kenya haitachukua mkondo wa Somalia na badala yake itapeleka kikosi cha usuluhishi wa kidiplomasia. Ifahamike kuwa Somalia ilitangaza kuuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Kenya usiku wa kuamkia Jumanne na kumrejesha balozi wake aliye Nairobi na kumtimua wa Kenyaaliyeko Mogadishu. Kwa mtazamo wake Somalia inashikilia kuwa Kenya inaingilia mambo yake ya ndani, madai ambayo jirani yake hajayapa uzito.

Yote hayo yakiendelea, Rais wa Somaliland Muse Abdi anakamilisha ziara yake rasmi ya kwanza nchini Kenya. Siku ya Jumanne amekutana na mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika, Raila Odinga, aliye pia kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM. Kupitia mtandao wake wa Twitter, Rais Muse alibainisha kuwa wamejadili mambo ya msingi na kubadilishana mawazo kuhusu juhudi za ushirikiano. Raila Odinga amekutana na Rais Muse wa Somaliland kwani kuimarisha uhusiano wa Kikanda ni moja ya majukumu yake kama mjumbe wa Umoja wa Afrika.

Somalia, Tabda: Soldaten aus Kenia
Wanajeshi wa Kenya walioko SomaliaPicha: picture-alliance/AP/B. Curtis

Ujio wa Rais wa Somalilandndio uliozua mtafuruku kati ya Kenya na Somalia kwani eneo hilo halitambuliki rasmi kimataifa kama nchi. Kwa upande wake, Somalia imetangaza kuwa inawapa wajumbe wa kidiplomasia wake na wa Kenya siku saba kurejea nyumbani.

Waziri wa mawasiliano wa Somalia Osman Dubbe aliyasema hayo usiku wa kuamkia Jumanne kupitia tangazo la televisheni ya taifa, SNTV. Hadi kufikia sasa Kenya inashikilia kuwa haijapokea waraka rasmi kutoka kwa Somalia kuhusu madai ya kuidhalililisha kidiplomasia.

Somalia inajiandaa kwa uchaguzi mkuu kadhalika vikosi vya pamoja vya Umoja wa Afrika vinavyolinda amani Mogadishu vinakamilisha muda wao wa kuhudumu mwakani. 

Ziara ya Rais wa Somaliland imekamiilika na yeye na mwenyeji wake wameafikiana kuwa na uwakilishi wa kidiplomasia kwenye miji ya Hargeisa na Nairobi ifikapo mwishoni mwa Machi mwakani. Miji hiyo itaunganishwa kwa safari za ndege za shirika la Kenya Airways na kampuni nyengine ifikapo wakati huohuo. Kadhalika mlango wa ushirikiano wa kiufundi na kiuchumi umefunguliwa. Hii ni ziara ya pili rasmi kufanywa na kiongozi wa Somaliland tangu mwaka 2009.