Ujerumani yapekua nyumba zinazohusishwa na harakati za Iran
16 Novemba 2023Wizara ya Mambo ya Ndani imesema Kituo cha Kiislamu cha Hamburg - IZH, kimekuwa kikifuatiliwa kwa muda mrefu na shirika la ujasusi la Ujerumani. Imesema harakati za kundi hilo zinalenga kueneza dhana ya kimapinduzi ya kiongozi wa juu wa Iran.
Maafisa pia wanachunguza kuhusu tuhuma kuwa kituo hicho kinaunga mkono shughuli zilizopigwa marufuku Ujerumani za kundi la wanamgambo wa Hezbollah la Lebanon linaloungwa mkono na Iran, ambalo limekuwa likishambuliana na Israel kwenye mpaka wa Israel na Lebanon tangu Hamas walipoishambulia Israel kutokea Gaza mwezi uliopita.
Taasisi ya IZH ina msikiti Hamburg. Misako ya jana ilifanywa Hamburg na majimbo mengine sita ya Ujerumani - Baden-Wuerttemberg na Bavaria katika upande wa kusini, Berlin, na Hesse, North-Rhine Westphalia na Lower Saxony katika upande wa magharibi na kaskazini magharibi.