1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujumbe wa UNSOM waombwa kuondoka Somalia

Angela Mdungu
10 Mei 2024

Serikali ya Somalia imeuomba Umoja wa Mataifa kusitisha shughuli za ujumbe wake wa kisiasa nchini humo. Ombi hilo limetolewa na waziri wa mambo ya kigeni kupitia barua yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/4fiVL
Somalia imeomba sujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa usitishe shughuli zake nchini humo
Rais wa Somalia Hassan Sheikh MohamudPicha: REUTERS

Uwakilishi huo wa kisiasa, UNSOM, ulikuwa ukiishauri serikali ya Somalia kuhusu masuala ya amani, mageuzi ya kiusalama na demokrasia kwa zaidi ya muongo mmoja.

Somalia imetoa ombi hilo la kuhitimisha shughuli za ujumbe huo wa kisiasa wa Umoja wa mataifa uliokuwa na wafanyakazi 360 mara tu muda wake utakapomalizika mwezi Oktoba mwaka huu. Maafisa watatu wa Umoja wa Mataifa wamethibitisha kuwepo kwa barua hiyo iliyoandikwa Mei 5, mwaka huu na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii Alhamisi wiki hii.

Katika barua hiyo, Waziri wa masuala ya kigeni wa Somalia Aimed Moa Fiji hakutoa sababu za Somalia kufikia uamuzi huo. Hata hivyo aliandika kuwa, serikali yake inaamini huu ni wakati sahihi wa kuelekea katika awamu mpya ya ushirika kati ya nchi hiyo na Umoja wa Mataifa. Naye mshauri wa rais wa nchi hiyo alithibitisha kuandikwa kwa barua hiyo ambapo kwa upande wake alisema kuwa Mogadishu haihitaji tena msaada wa Umoja wa mataifa kuratibu masuala baina yake na jumuiya ya kimataifa .

Soma zaidi: Hali ya haki za binadamu Somalia inatia wasiwasi

Licha ya kauli hiyo mshauri huyo wa rais alibainisha kuwa ujumbe huo wa UNSOM umekuwa na matumizi makubwa ambayo kwa mwaka ni karibu dola milioni 100 za Kimarekani. 

Somalia imewasilisha katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ombi la kutaka kuuondoa ujumbe wa UNSOM nchini humo
Somalia imewasilisha katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ombi la kutaka kuuondoa ujumbe wa UNSOM nchini humoPicha: Loey Felipe/UN Photo/Xinhua/picture alliance

Mwisho wa shughuli za ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa ni tofauti na Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika ulio chini ya Umoja wa Mataifa wenye zaidi ya wanajeshi 10,000 nchini humo. Ujumbe huo pia unatarajiwa kuondoka nchini humo na kukabidhi mamlaka yake kwa serikali ya Somalia mwishoni mwa mwaka huu.

Somalia ilituhumu UNSOM kwa kuingilia masuala yake ya ndani

Mchambuzi wa siasa za Somalia Matt Bryden, amebainisha kuwa serikali ya nchi hiyo iliwahi kuutuhumu uwakilishi huo wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa kwa kuingilia masuala ya ndani ya Somalia.

Ni wakati Rais wa nchi hiyo Hassan Sheikh Mohamud, akiwa katika harakati za kuipa mamlaka zaidi serikali kuu kwa kuifanyia katiba mageuzi na mabadiliko mengine. Lakini ujumbe wa UNSOM  umekuwa ukijaribu kupata uwiano kati ya ajenda ya serikali kuu na matamanio ya majimbo nchini humo kuwa na mamlaka zaidi.

Wakati Somalia ikikabiliwa na mgogoro tangu mwaka 1991 ikiwa ni pamoja na makundi ya wanamgambo wanaohusishwa na kundi la al qaeda, mamlaka za Somalia zimechukua hatua ya kurejesha huduma na usalama. Taifa hilo lenye watu milioni 17 linasalia kuwa miongoni mwa nchi zenye vurugu na masikini zaidi duniani.