Ujumbe wa UN kuondoka Irak mwishoni mwa mwaka 2025
1 Juni 2024Uamuzi huo umechukuliwa baada ya Umoja wa Mataifa kupokea ombi la kumaliza kazi za ujumbe huo kutoka kwa serikali mjini Baghdad.
Serikali ya Iraq imekaribisha uamuzi huo ikisema unaashiria maendeleo na uthabiti uliopo nchini humo tangu Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi wa Irak UNAMI ulipoundwa mwaka 2003, baada ya uvamizi ulioongozwa na Marekani kuuangusha utawala wa kiongozi wa zamani Sadam Hussein.
Waziri Mkuu wa Irak ataka kikosi cha Marekani kiondoke nchini humo
Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha uamuzi huo hapo jana Ijumaa na kuongeza muda wa ujumbe huo hadi tarehe 31 Desemba mwaka 2025 ambako UNAMI itasitisha kazi zake zote nchini Irak.
Ujumbe huo unao wafanyakazi takriban 700 ambao kazi yake ni kuishauri serikali kuhusu mazungumzo ya kisiasa na maridhiano pamoja na kusaidia katika masuala ya uchaguzi na mageuzi ya kiusalama.