Ukraine yasifu Bunge la Marekani kuidhinisha msaada mpya
21 Aprili 2024Baraza hilo lilipitisha bila vizingiti msaada wa kiasi dola bilioni 95 unaojumuisha kitita kwa ajili ya Ukraine, Israel na washirika wengine wa Marekani duniani.
Uamuzi huo uliochelewa kwa miezi kadhaa ulifikiwa katika kura iliyoungwa mkono na vyama vyote viwili nchini Marekani. Unafuatia upinzani mkubwa kutoka kwa wanasiasa wanaoonesha kuchoshwa na kuipatia fedha zaidi Ukraine kupambana dhidi ya vikosi vya Urusi.
Chini ya msaada huo, Ukraine itapatiwa dola bilioni 61 kiasi kinachotazamiwa kitasaidia pakubwa kurejesha matumaini ya vikosi vya nchi hiyo ambavyo miezi ya karibuni inaonesha vimezidiwa nguvu na vile vya Urusi.
Maafisa nchini Ukraine wamekuwa wakitahadharisha kwamba nchi hiyo itapoteza udhibiti kwenye uwanja wa vita iwapo mataifa washirika hayatatuma silaha, mifumo ya ulinzi na misaada mingine kulifikia jeshi lake.
Zelenskyy: Marekani imeonesha uongozi wa dhati kuisaidia Ukraine
Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine ambaye amekuwa akitoa shinikizo kubwa kwa washirika wake hasa Marekani, amesema amefarijika sana na uamuzi wa wabunge wa Marekani.
"Tunathamini kila ishara ya uungaji mkono kwa nchi yetu na uhuru wake, watu na mtindo wetu wa maisha, ambao Urusi inajaribu kuuzika kwenye kifusi," aliandika kiongozi huyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X.
"Marekani imeonesha uongozi wake tangu siku za mwanzo za vita, Hii ndiyo aina ya uongozi unaohitajika kuleta uthabiti wa mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria na kutabirika kwa kila taifa," aliongeza kiongozi huyo.
Zelensky amesema wapiganaji wa nchi yake walio mstari wa mbele wataiona faida ya msaada huo wa Marekani.
Viongozi wengine wa nchi washirika watoa neno kupitishwa msaada
Viongozi kadhaa wa nchi za magharibi pia wamesifu hatua ya kupitishwa msaada huo kwa ajili ya Ukraine.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami, NATO, Jens Stoltenberg,amesema Ukraine imekuwa ikitumia silaha zilizotolewa na wanachama wa mfungamano huo wa kijeshi kusambaratisha uwezo wa vikosi vya Urusi.
Kwa mtazamo wake mapambano hayo ya Ukraine yameyawezesha mataifa wanachama wa Ulaya na Amerika Kaskazini kuwa salama zaidi.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema "Ukraine inahitaji msaada wote inaoweza kuupata ili ipambane na Urusi."
Tamko lake limeungwa mono pia na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani ambaye amesema "ni ishara nzito katika nyakati hizi" na kwamba wanasimama pamoja na Ukraine inayopigania "uhuru, demokrasia na haki ya kujitawala."
Urusi yaonya kuzidi kuisadia Ukraine, vikosi vyake vyadai kusonga mbele
Nchini Urusi, msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema kuidhinishwa kwa msaada huo kwa Ukraine kulitarajiwa, aliongeza kuwa uamuzi huo utaitajirisha zaidi Marekani, na kuiharibu zaidi Ukraine na kusababisha vifo vya maelfu na maelefu zaidi ya Waukraine.
Naye msemaji wa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Urusi, Maria Zakharova pia alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuzungumzia msaada huo.
"Kutolewa msaada wa kijeshi na Marekani kwa Ukraine, Israel na Taiwan kutaongeza mzozo duniani: msaada wa kijeshi kwa utawala wa Kyiv ni ufadhili wa moja kwa moja wa shughuli za kigaidi," alindika Bibi Zakharova kupitia mtandao wa Telegram.
Mamtashi mengine yametoka kwa mkuu wa kamati ya mambo ya kigeni ya bunge la Urusi, Duma, Leonid Slutsky, ambaye amesema "Msaada mpya hautanusuru chochote badala yake utawaua maelfu ya watu, kuurefusha mzozo na kuongeza janga na uharibifu."
Katika hatua nyingine Urusi imesema vikosi vyake vimekikamata kijiji kilicho mstari wa mbele wa mapambano cha Bogdanivka. Kinapatikana kiasi kiasi tatu kutoka mji ulio chini ya udhibiti wa vikosi vya Ukraine wa Chasiv Yar.
"Vikosi vyetu upande wa kusini vimelikomboa eneo la Bogdanivka," imesema taarifa ya wizara ya ulinzi ya Urusi.