Ulimwengu waendeleza juhudi za kuzuia kuenea kwa COVID-19
17 Machi 2020Akizungumza na waandishi habari, baada ya kuwaarifu viongozi wa kundi la nchi saba zilizoendelea zaidi kiuchumi duniani, G7 kuhusu pendekezo lake, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, amesema marufuku hiyo inaweza kuwekwa katika siku zijazo ili kukabiliana na mzozo wa kiafya unaoendelea ulimwenguni. Amesema anatarajia viongozi wa Umoja wa Ulaya watalikubali pendekezo hilo katika mkutano wa dharura unaofanyika Jumanne kwa njia ya video.
Watakaokiuka marufuku kulipa faini
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron ameamuru wananchi kubakia majumbani na kwamba mipaka yote ya Ufaransa itafungwa kwa muda wa siku 30 zijazo. Macron ambaye ametangaza kuwa dunia iko katika ''vita ya kiafya'' amesema kuanzia Jumanne watu wataruhisiwa tu kutoka nyumbani kwa ajili ya shughuli muhimu kama vile kununua chakula na kwenda kazini.
Ufaransa itawatawanya polisi 100,000 ili kufuatilia mienendo ya watu na wale watakaobainika kukiuka marufuku iliyowekwa watatozwa faini ya hadi Euro 135.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel ametangaza kusimamishwa kwa shughuli za kijamii, huku nchi hiyo ikiwa imeanza kuifunga mipaka yake. Akilihutubia taifa kuhusu virusi vya corona mjini Berlin, Merkel amesema maduka ya vyakula, vituo vya mafuta, benki na maduka ya dawa yataendelea kufunguliwa, huku maduka yanayouza bidhaa zisizo muhimu yatafungwa.
Merkel amesema migahawa nchini Ujerumani itafungwa kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa kumi na mbili asubuhi. Hayo ameyathibitisha baada ya kufikiwa makubaliano kati ya serikali za majimbo na serikali ya shirikisho. Amebainisha kuwa kumbi zote za starehe, baa, sinema, mabwawa ya kuogelea, maeneo ya michezo ya watoto pamoja na bustani za wanyama zote zitafungwa.
Merkel amesema safari zote za likizo ndani na nje ya nchi zimesitishwa kwa sasa. Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier amewasihi wananchi wote kubakia majumbani, baada ya serikali kutangaza marufuku ya nchi nzima ili kupunguza kuenea kwa COVID-19.
Wataalamu: Wengi kuambukizwa Uholanzi
Waziri Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte amesema wataalamu wa afya wamewaarifu kuwa idadi kubwa ya watu wa nchi hiyo wataambukizwa virusi vya corona na kwamba janga hilo litakuwa gumu, lakini kwa pamoja watafanikiwa kulishinda.
Shirika la Afya Duniani, WHO limezitaka nchi zote kuongeza mipango ya upimaji wa virusi vya Corona ili dunia iweze kufanikiwa zaidi katika kukabiliana na janga hilo. Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ameukataa wito huo wa WHO wa kuanzisha mpango wa kuwapima watu.
Johnson pia amekataa wito wa kuzifunga shule na amesema wanachokifikiria kwa sasa ni kuendelea kuzifungua shule hizo. Aidha, waziri huyo mkuu wa Uingereza amesema kulikuwa na makubaliano kati ya viongozi wa kundi la G7 kwamba kunapaswa kuwa na fedha kwa ajili ya kuzisaidia nchi zitakazoathirika kiuchumi kutokana na virusi hivyo.
Rais wa Marekani, Donald Trump amewaonya Wamarekani kwamba huenda wakatumbukia katika mdororo wa kiuchumi kutokana na virusi vya corona. Hofu ya Trump imejitokeza baada ya soko la hisa la Marekani la Wall Street kuripoti kuhusu kushuka vibaya kwa mauzo, katika siku ambayo halijawahi kushuhudia kwa zaidi ya miongo mitatu.
Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limefuta mikutano yake yote iliyopangwa kufanyika wiki hii.
Idadi ya watu waliokufa kutokana na virusi vya corona katika nchi 145 ulimwenguni imefikia 7,126 huku watu 181,546 wakiwa wameambukizwa virusi hivyo na wengine 78,088 wakiwa wamepona.
(AP, DPA, DW https://bit.ly/2wZVD27)