DRC yatakiwa kuiruhusu MONUSCO kupambana na FDLR
24 Februari 2015Wito huo umetolewa na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika katika kikao chake cha kuujadili mzozo wa Kongo, kilichofanyika jana mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika katika ukanda wa Maziwa Makuu, Boubacar Gaoussou Diarra, amesema ili operesheni ya kupambana na waasi wa kundi la Kihutu kutoka Rwanda-FDLR iweze kufanikiwa, mapambano inabidi yafanyike kwa ushirikiano kati ya majeshi ya Kongo na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo-MONUSCO.
Diarra amesema wanataka kuona Kongo inafaidika na msaada wa vifaa na operesheni kutoka kwa MONUSCO. Amesema hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha operesheni hiyo inafanikiwa dhidi ya kundi la FDLR, kwa sababu waasi hao wamekuwepo nchini Kongo kwa zaidi ya miaka 20 na wamejipenyeza hadi kwenye maeneo wanakoishi watu.
Kikosi cha MONUSCO kilikuwa kiko tayari kuyasaidia majeshi ya Kongo kupambana na FDLR, lakini kilisitisha msaada wake huo mapema mwezi huu, kwa sababu majenerali wawili waliokuwa wameteuliwa kuongoza operesheni hiyo wanakabiliwa na tuhuma za kukiuka haki za binaadamu.
Wiki iliyopita, Rais wa Kongo, Joseph Kabila alisema operesheni hiyo imeanza bila ya msaada wa MONUSCO.
Majenerali hao walitakiwa kuondolewa katikati ya mwezi huu
Umoja wa Mataifa uliipia Kongo muda wa hadi katikati ya mwezi huu wa Februari, iwe imewaondoa majenerali hao wawili Bruno Mandevu na Fall Sikabwe, ambao wanatuhumiwa kuhusika na ukiukaji wa haki za binaadamu.
Hata hivyo, serikali ya Kongo imesema kikosi cha Umoja wa Mataifa hakijaonyesha ushahidi wowote kuhusu shutuma hizo na kwamba haina taarifa kuhusu ukiukwaji wowote wa haki za binadaamu uliofanywa.
Januari 8 mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliunga mkono hatua ya kikosi cha MONUSCO kusaidia katika operesheni za kupambana na waasi wa FDLR wanaokisiwa kuwa 1,400, wakiwemo wanajeshi wa zamani wanaohusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
Kundi hilo lilikaidi amri ya kusalimisha silaha Januari Pili mwaka huu, tarehe ambayo ilikuwa imewekwa kwa ajili ya kuweka chini silaha hizo.
Wakati huo huo, Ripoti iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa imetaka ndege zisozi na rubani zipelekwe kwenye maeneo ambako kuna idadi kubwa ya vikosi vyake vya kulinda amani, kama sehemu ya kukabiliana na mizozo duniani. Mkuu wa jopo la watu watano walioiandaa ripoti hiyo, Jane Hotte Lule, amesema hiyo ni teknolojia muhimu kwa majeshi ya ardhini.
Kikosi cha MONUSCO kilichoko nchini Kongo, ndicho kikosi kikubwa zaidi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, na kimekuwa kikitumia ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kuwafatilia waasi walioko eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman