Umoja wa Afrika wasimamisha uanachama wa Gabon
1 Septemba 2023Siku ya Alhamisi (31.08.2023) baraza la amani na usalama la Umoja huo, lilisema kuwa linalaani vikali mapinduzi hayo yaliomuondoa madarakani rais Ali Bongo. Wiki chache zilizopita, Umoja huo wa Afrika pia ulisimamisha uanachama wa Niger baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai.
Soma pia:Umoja wa Ulaya wasema hakuna mipango ya kuwaondoa raia wa nchi za umoja huo kutoka Gabon.
Uanachama wa Burkina Faso, Mali, Guinea na Sudan katika Umoja huo pia umesimamishwa tangu mapinduzi ya kijeshi katika mataifa hayo.
Umoja wa Ulaya unapinga mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon
Katika hatua nyingine, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema kuwa Umoja huo unapinga kutwaliwa kwa nguvu kwa mamlaka nchini Gabon. Katika taarifa hapo jana, Borrell amesema kuwa changamoto zinazoikabili Gabon lazima zitatuliwe kulingana na kanuni za sheria, utaratibu wa kikatiba na demokrasia.
Soma pia:Viongozi wa Afrika kujibu hatua ya mapinduzi ya kijeshi Gabon
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa amani na ustawi wa taifa hilo pamoja na utulivu wa kikanda unategemea masuala hayo. Borrell ametoa wito wa mazungumzo jumuishi na madhubuti badala ya nguvu ili kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu na matakwa ya raia wa Gabon.
Maafisa wa jeshi watangaza kuvunjwa kwa taasisi zote za serikali
Jeshi lilipindua serikali ya Gabon mapema Jumatano (30.08.2023). Maafisa wa jeshi hilo walitangaza kupitia televisheni ya taifa kwamba taasisi zote za serikali zimevunjwa, matokeo ya uchaguzi wa hivi karibuni kufutwa kwasababu ya dosari za uchaguzi na mipaka ya nchi hiyo kufungwa.
Soma pia:Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Afrika walaani mapinduzi ya kijeshi Gabon
Muda mfupi kabla ya mapinduzi hayo, maafisa wa uchaguzi walikuwa wamemtangaza Bongo ambaye amekuwa uongozini tangu mwaka 2009, mshindi wa uchaguzi huo wa Agosti 26. Jumatano jioni, viongozi wa kijeshi, walimtaja mkuu wa ulinzi wa rais Brice Clotaire Oligui Nguema kama kiongozi wa mpito wa taifa hilo.