1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika wataka mapigano yasitishwe Tigray, Ethiopia

10 Novemba 2020

Umoja wa Afrika umetoa wito wa kusitishwa mapigano kwenye eneo la kaskazini mwa Ethiopia, ambako majeshi ya serikali ya shirikisho yanapigana na vikosi vya jimbo la Tigray.

https://p.dw.com/p/3l6gC
Unruhen in Äthiopien
Picha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ametoa wito wa kufanyika mazungumzo ya amani pamoja na kusitishwa mapigano kwenye jimbo la Tigray ambako imeripotiwa kuwa majeshi ya serikali yameutwaa uwanja wa ndege.

Mahamat amehimiza kukomeshwa kwa uhasama na amezitaka pande zinazohusika kuheshimu haki za binaadamu na kuhakikisha ulinzi wa raia.

Wanajeshi Tigray wajisalimisha

Vikosi vya serikali ya jimbo la Tigray vilijisalimisha wakati wa kutekwa kwa uwanja wa ndege wa Humera, ulioko karibu na mpaka wa Sudan na Eritrea, huku jeshi la serikali ya shirikisho pia likiidhibiti barabara kuu inayoelekea kwenye mji uliopo kwenye mpaka wa Sudan.

Akizungumzia suala la kujisalimisha, mpiganaji wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray, TPLF ambaye hakutaka kutajwa jina amesema wamefurahia kupelekwa kwa majeshi ya serikali.

Moussa Faki Afrikanische Union
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki MahamatPicha: Mahmoud Hjaj/picture alliance/ AA

"Nimejisalimisha kwa jeshi, sababu sio lazima tuingie kwenye vita kwa madai ya uongo. Tunapaswa kuutetea na kuulinda umoja wa taifa letu. Hivyo, vijana wa jimbo la Tigray hawapaswi kuingia vitani, alifafanua mpiganaji huyo.

Waziri Mkuu, Abiy Ahmed aliyeshinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019, aliamuru kufanyika kwa mashambulizi ya anga na kupeleka majeshi Tigray wiki iliyopita akikituhumu chama cha TPLF kwa kuishambulia kambi ya kijeshi.

Wakati hayo yakijiri, kiongozi wa Tigray, Debretsion Gebremichael amedai Eritrea imewapaleka wanajeshi wake eneo la mpakani, ili kuvishambulia vikosi vyake, wakiiunga mkono serikali ya Ethiopia. Hata hivyo, Gebremichael hakutoa ushahidi wowote.

Aidha, serikali ya Eritrea imekanusha madai hayo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Eritrea, Osman Saleh Mohammed amesema mzozo unaoendelea Ethiopia ni wa ndani na wao sio sehemu ya mzozo huo.

Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed Picha: Minasse Wondimu Hailu/picture alliance/AA

Abiy amesema anaamini kuwa anaweza kuutuliza mzozo wa Tigray kwani uko mbioni kudhibitiwa. Katika ukurasa wake wa Twitter, waziri mkuu huyo ameandika leo Jumanne kuwa shughuli za utekelezaji wa sheria huko Tigray zinaendelea kama ilivyopangwa.

Amesema operesheni zitasitishwa mara moja baada ya serikali ya kijeshi isiyo halali itakaponyang'anywa silaha na utawala halali kwenye eneo hilo utakaporudishwa madarakani na wahusika waliokamatwa watakapofikishwa mahakamani.

Ama kwa upande mwingine serikali ya Sudan imesema maelfu ya Waethiopia wanaoukimbia mzozo huo wamevuka mpaka na kuingia kwenye nchi hiyo jirani. Mkuu wa shirika la kuwahudumia wakimbizi nchini Sudan, Alsir Khaled amesema takriban wakimbizi elfu tatu wameingia kwenye mji wa Kassala.

 

(AFP, AP, Reuters)