1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yafanya mashambulizi ya angani Tigray

9 Novemba 2020

Waziri mkuu wa Ethiopia ameimarisha operesheni ya kijeshi katika jimbo la kaskazini la Tigray kwa kufanya mashambulizi ya anga ambayo ni sehemu ya kile alichokiita kuwa operesheni ya kuleta utiifu wa sheria.

https://p.dw.com/p/3l2uR
Äthiopien Adwa Tigray
Picha: Yared Shumete

Mnamo Jumapili, mashambulizi ya anga yalikuwa sehemu ya operesheni ya kijeshi ya serikali kuu dhidi ya jimbo la Tigray na kuongeza hofu ya kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Waziri mkuu Aby Ahmed amekataa katakata kusikiliza miito kutoka Umoja wa Mataifa na washirika wake katika ukanda huo wa kumtaka akae kwenye mazungumzo na viongozi wa jimbo hilo la Tigray, jimbo ambalo linakaliwa na jamii ya kabila lililowahi kuihodhi serikali kuu mjini Addis kabla ya Abiy kuingia madarakani mwaka 2018.

Soma pia: Ethiopia yakusudia kuondoa uongozi wa jimbo la Tigray

''Nyuma ya migogoro iliyosababisha madhila na vifo vya waethiopia wengi katika kipindi cha miaka miwili iliyopita,wafuatiliaji wa karibu wa siasa za Ethiopia wanaweza kuona wazi ushawishi wa kundi hili la TPLF.Linafadhili,kutoa mafunzo na silaha kwa kikosi chochote kilichotayari kuingia kwenye vurugu na vitendo visivyokuwa halali kuhujumu kipindi cha mpito. Lengo lao lilikuwa wazi ni kuifanya nchi hii isiweze kuwa na uongozi kwa kuchochea mapigano kwa misingi ya kikabila na kidini,na kuongeza migawanyiko na mtengano ili kipindi cha mpito cha demokrasia kipoteze nguvu zake.'' Amesema Abiy.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Ethiopia Broadcasting Corporation//REUTERS

Ikumbukwe kwamba waziri mkuu Abiy wiki iliyopita alianzisha operesheni hii ya kijeshi katika jimbo hilo akisema kwamba vikosi vitiifu kwa viongozi wa Tigray viliishambulia kambi ya jeshi la serikali kuu na kujaribu kupora vifaa. Waziri mkuu Abiy anawashutumu viongozi wa jimbo hilo kwa kuhujumu mageuzi yake ya kidemokrasia.

Soma pia: Ethiopia yashinikizwa kusitisha operesheni ya kijeshi Tigray

Ndege za kijeshi za serikali toka wakati huo zimekuwa zikishambulia maeneo ya jimbo hilo ambalo linapakana na Sudan na Eritrea na jana jumapili wafanyakazi wa mashirika ya msaada walisema kwamba mapigano makali yalishuhudiwa katika maeneo chungu nzima ya jimbo hilo ambapo kiasi watu sita waliuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Lakini pia mnamo Jumapili, waziri mkuu Abiy alimtangaza mkuu mpya wa majeshi,mkuu wa ujasusi na kamishna mkuu mpya wa jeshi la polisi pamoja na waziri wa mambo ya nje. Wachambuzi wanasema katika mabadiliko hayo Abiy amewaweka kwenye ngazi za juu washirika wake wa wakati mgogoro ukiwa unashika kasi.

Kiongozi huyo wa Ethiopia alitunukiwa mwaka jana tuzo ya amani ya Nobel kwa jitihada zake za kuleta amani na jirani yake Eritrea na pia kwa kuanzisha mageuzi ya kidemokrasia nchini mwake,lakini shirika la kimataifa linalofuatitilia migogoro ICG limeonya kwamba kipindi hicho cha mpito cha demokrasia aliyoahidi kinatishiwa na mgogoro huu wa Tigray.

Takriban watu milioni 9 wanaoishi karibu na mipaka ya jimbo hilo la Tigray wako katika hatari kubwa kufuatia mgogoro huu.

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW