Ethiopia yakusudia kuuondoa uongozi wa jimbo la Tigray
7 Novemba 2020Kura hiyo ya tawi la juu la bunge haihitaji kuidhinishwa kwenye ngazi yoyote zaidi ya hapo na inampa Waziri Mkuu Abiy Ahmed uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya uongozi wa Tigray pale serikali yake inapojiridhisha kuwa uongozi huo umekiuka sheria.
Serikali ya shirikisho la Ethiopia imesema utawala wa mpito utateua maafisa, watakaokuwa na jukumu la kuhakikisha sheria inaheshimiwa, kuidhinisha bajeti ya mkoa huo pamoja na kuandaa mchakato wa kuendesha uchaguzi.
Soma zaidi:Gutteres atoa wito wa kusitishwa mapigano Tigray, Ethiopia
Katika taarifa mpya iliyotolewa Jumamosi, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel waziri mkuu Abiy Ahmed amesema wahalifu hawawezi kuepuka sheria chini ya mwamvuli wa kutafuta mapatano na wito wa kufanyika mazungumzo.
Kwa upande mwingine taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wa Facebook wa serikali ya jimbo la Tigray, chama cha Tigray People's Liberation Front, (TPLF) kimesema kitashinda vita vya kutetea haki yao na chama hicho kimeandika pia kwenye ujumbe huo kuwa "mpiganaji hatajadiliana na maadui zake " huku kikijisifu kuwa Watigray wanamiliki silaha za kisasa.
Wataalam na wanadiplomasia wanaingalia hali hiyo kwa mshangao na wasiwasi wakati pande mbili zinazo miliki silaha nzito majeshi yao yakiwa yanapambana katika eneo hilo la Upembe wa Afrika.
Upinzani watoa kauli
Mvutano huo umezusha hofu kwamba nchi hiyo inaweza kuingia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Nchi hiyono moja wapo yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika ikiwa na wakazi wapatao milioni 110. Mpaka sasa hakuna upande unaoonekana kuridhia juu ya kufanyika mazungumzo ambayo wataalam wamesema yanahitajika ili kuepuka maafa.
Inahofiwa pia kwamba mzozo wa nchini Ethiopia unaweza ukahatarisha usalama wa nchi jirani za Sudan, Eritrea na Somalia. Wakati hayo yakiendelea nchini Ethiopia Waziri Mkuu wa Sudan, Abdalla Hamdok amezungumza kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ambaye ameelezea wasiwasi wake juu ya hali inayoendelea nhini Ethiopia.
Wakati huo huo shirika la habari la Sudan limeripoti kwamba nchi hiyo imefunga mipaka yake katika mkoa wa al-Qadarif mashariki mwa Sudan inayopakana na mikoa ya Tigray na Amhara katika nchi jirani ya Ethiopia.
Soma Zaidi:Ethiopia yashinikizwa kusimamisha kampeni ya kijeshi Tigray
Mzozo ulizuka siku chache zilizopita kati ya serikali ya shirikisho ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed na washirika wake wa zamani wa utawala wa jimbo la Tigray, baada ya Abiy kutuma vikosi vya kijeshi katika eneo hilo. Abiy anakishutumu chama cha ukombozi wa watu wa Tigray (TPLF) kwa kufanya mashambulizi katika kambi ya jeshi la shirikisho kwa lengo la kuiba vifaa vya kivita.
Kwa muendelezo huo serikali kuu ya Ethiopia imetangaza hali ya hatari kwa muda wa miezi sita na katika kipindi hicho ni marufuku kuweko mikusanyiko ya watu, na mizunguko imezuiwa.
Vyanzo: (AP/DPA)